WIZARA YA AFYA YATATHMINI UTAYARI WA WATUMISHI WA AFYA PERAMIHO KUKABILIANA NA EBOLA
Posted on: November 2nd, 2026Na Happyness Hans, WAF - Ruvuma
Mratibu wa Magonjwa ya Dharura, Maafa na Magonjwa ya Milipuko, Bi. Theresia Haule, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Shirika la Afya Duniani (WHO), imefanya tathmini ya utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko katika Mkoa wa Ruvuma, hususan ugonjwa wa Ebola, kwa lengo la kuhakikisha watumishi wa afya katika hospitali za Serikali na binafsi wanakuwa na uelewa na uwezo wa kujikinga na kudhibiti maambukizi.
Akizungumza leo Novemba 2, 2026 Mkoani Ruvuma. Bi. Theresia Haule amesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na umuhimu wa kuimarisha utayari wa Mkoa wa Ruvuma, ambao unapakana na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidekrasia ya Kongo(DRC ) inayokabiliwa na ugonjwa wa Ebola hivyo ni muhimu kuwajengea uwezo watumishi wa afya ili waweze kutambua na kuchukua hatua stahiki endapo kutatokea mgonjwa anayeshukiwa kuwa na Ebola nchini.
Aidha, Bi. Haule amesema zoezi hilo ni endelevu na timu ya Wizara ya Afya itaendelea kutembelea mikoa yenye hatari kubwa ya kukumbwa na magonjwa ya milipuko, hususan ile iliyopo karibu na mipaka, ili kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, kinga na udhibiti wa maambukizi.
“Tunataka watumishi wa afya wawe na utayari na uelewa mkubwa katika kumtambua mtu anayeshukiwa kuwa na Ebola ili kurahisisha hatua za kujikinga na kuzuia maambukizi kuenea kwa watu wengine.”
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya St. Joseph Peramiho, Dkt. Adeodatus Haule ameishukuru Wizara ya Afya kwa kutembelea hospitali hiyo na kufanya tathmini ya utayari wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko, hususan Ebola.
Amesema wataalamu hao wametembelea maeneo mbalimbali ya hospitali na kutoa ushauri kuhusu mpangilio sahihi wa vifaa na maeneo ya huduma ili kuimarisha maandalizi ya kumhudumia mtu anayeshukiwa kuwa na Ebola.
Amesema kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kunahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya hospitali za Serikali, binafsi na za taasisi za dini hivyo ujio wa wataalamu hao umewasaidia kutambua maeneo yanayohitaji kuimarishwa na kuongeza utayari wa hospitali katika kuzuia na kudhibiti maambuki