WIZARA YA AFYA, WHO WAONGEA LUGHA MOJA MABORESHO HUDUMA ZA AFYA NCHINI
Posted on: November 2nd, 2026Na Aisha Swahibu, WAF – Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kuboresha huduma za afya nchini, huku ikitajwa kuwa ushirikiano huo una msingi imara uliowezesha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya afya.
Akiongea katika kikao cha pamoja kati ya Wizara ya Afya na WHO, Dr. Alex Gasasira
Mwakilishi mkazi wa WHO Tanzania, leo November 01, 2026, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Bruno Sunguya, ameipongeza timu za wataalamu kutoka pande zote mbili kwa juhudi na mchango wao katika kutekeleza mipango mbalimbali ya afya, huku akieleza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuendelezwa kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa na matokeo chanya kwa wananchi.
Prof. Bruno amesema Serikali inaendelea kuhitaji ushahidi wa kisayansi na tafiti zinazoweza kutumika kwa kuboresha sera, miongozo na utoaji wa huduma za afya, hivyo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha matumizi ya tafiti katika utekelezaji wa huduma za afya ili kuhakikisha maamuzi yanayofanywa yanakuwa na tija kwa wananchi.
Aidha, ameeleza kuwa ni muhimu kupitia miongozo ya WHO inayohusu huduma za afya na kutathmini namna inavyotekelezwa nchini, ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuhakikisha miongozo hiyo inazingatia mazingira na mahitaji ya Tanzania.
Katika hatua nyingine, Prof. Bruno amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ubora wa huduma za afya kwa kuzingatia uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miundombinu, vifaa tiba na mafunzo ya watumishi wa afya, akieleza kuwa uwekezaji huo unapaswa kuendana na matokeo bora ya huduma kwa wagonjwa.
Kwa upande wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Prof. Bruno amesema kuwa Serikali inaendelea kuweka kipaumbele katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, hivyo amehimiza kuendelezwa kwa juhudi zilizopo ili kudumisha mafanikio yaliyopatikana na kuhakikisha huduma za afya ya uzazi na mtoto zinaendelea kuboreshwa.
Vilevile, ameeleza kuwa maboresho ya huduma za tiba, hususan kwa wagonjwa wa kiharusi na majeruhi wa ajali za barabarani, ni maeneo muhimu yanayohitaji kupewa kipaumbele