Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA, UNICEF KUIMARISHA USHIRIKIANO KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NA LISHE

Posted on: November 2nd, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF - Dodoma

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) katika kuboresha huduma za afya ya msingi, lishe na huduma bora za afya kwa wananchi.

Prof. Sunguya ameyasema hayo leo Novemba 01, 2026, jijini Dodoma katika kikao na UNICEF kilichojadili maeneo ya ushirikiano, changamoto za utekelezaji wa afua za afya na namna ya kutumia utaalamu na ushahidi wa kisayansi kuimarisha huduma zinazotolewa nchini.

Amesema ni muhimu kwa wataalamu wa Wizara ya Afya na UNICEF kuwasiliana na kufanya kazi kwa karibu kupitia mikutano ya mara kwa mara ili kutatua changamoto za kiufundi na kuhakikisha shughuli zinazokubaliwa zinatekelezwa kwa ufanisi.

Aidha, Prof. Sunguya amewataka Wakurugenzi wa Wizara ya Afya kushirikiana moja kwa moja na wataalamu wa UNICEF katika maeneo yao ya kitaalamu, badala ya kusubiri kila suala kufikishwa kwa viongozi wa juu, ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli za pamoja.

Katika kikao hicho, washiriki pia walijadili matokeo ya tafiti zilizofanyika kuhusu gharama za utoaji wa huduma za afya ya msingi, namna ya kuboresha ufanisi wa matumizi ya rasilimali zilizopo serikalini na uwezekano wa kupata rasilimali zaidi kwa ajili ya kuimarisha huduma hizo.

Akizungumzia vipaumbele vya sekta ya afya, Prof. Sunguya ametaja uboreshaji wa ubora wa huduma za afya, kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza, kuimarisha huduma kwa wagonjwa wa kiharusi na kupunguza athari za ajali za barabarani.

Katika upande wa lishe, amesema ni eneo muhimu linalohitaji kupewa kipaumbele, hususan katika kukabiliana na upungufu wa damu kwa vijana balehe, akieleza umuhimu wa kushirikisha sekta ya elimu katika kuimarisha afua za lishe mashuleni.

Vilevile, majadiliano yaligusia umuhimu wa kutathmini afua mbalimbali za kukabiliana na upungufu wa virutubishi mwilini, ikiwemo matumizi ya virutubishi vya kuongeza damu, ulaji unaofaa na uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula, kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi na mahitaji ya makundi husika.