Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA, MKAPA FOUNDATION KUIMARISHA USHIRIKIANO MAFUNZO NA HUDUMA AFYA NCHINI

Posted on: November 2nd, 2026


Na Aisha Swahibu, WAF - Dodoma

Wizara ya Afya na Benjamin William Mkapa Foundation (BMF) imeendelea kuimarisha ushirikiano katika kuongeza upatikanaji wa wataalamu wa afya na kuboresha huduma za urekebishaji wa afya nchini.

Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Bruno Sunguya, akimwalisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe leo Novemba 03, 2026 wakati wa kikao na wajumbe wa bodi ya Benjamin William Mkapa Foundation, jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa, licha ya Serikali kuendelea kuwekeza katika mafunzo ya wataalamu kupitia programu mbalimbali, mahitaji ya wataalamu bingwa bado ni makubwa na yanahitaji ushirikiano wa wadau ili kuongeza fursa za mafunzo na kuimarisha upatikanaji wa wataalamu katika maeneo yenye uhitaji.

Aidha, Prof. Sunguya amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika huduma za urekebishaji wa afya (rehabilitation), hususan kwa wagonjwa waliopata kiharusi, majeraha yatokanayo na ajali na watu wenye mahitaji maalumu ya urekebishaji, akibainisha kuwa huduma hizo zinahitaji wataalamu wenye ujuzi na uwezo wa kutosha katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Prof. Sunguya amesema kuimarisha mafunzo ya wataalamu wa tiba ya viungo, tiba ya usemi na kada nyingine za urekebishaji kutasaidia kuongeza uwezo wa mfumo wa afya kutoa huduma zinazowawezesha wagonjwa kurejesha uwezo wa kufanya shughuli zao za kila siku.

Pia, ameitambua nafasi ya wadau katika kuendeleza programu zenye manufaa kwa wananchi, ikiwemo huduma kwa watoto wenye tatizo la mguu kifundo (clubfoot).

Vilevile, Prof. Sunguya amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kupima ubora wa huduma na kupata mrejesho kutoka kwa wagonjwa na wateja wa huduma za afya katika ngazi mbalimbali, ili kubaini changamoto na kuweka maboresho yanayozingatia mahitaji halisi ya wananchi.

“Eneo la Ubora wa Huduma ni kipaumbele cha Waziri wetu wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa hivyo Wizara tukiunga nguvu kwa pamoja na wadau wote wa sekta ya afya kwenye kuja na mfumo sahihi kidigitali tunaweza kufikia lengo na adhma hii ya Mhe. Waziri,” amesema Prof. Sunguya