Wizara Ya Afya

WAZIRI MCHENGERWA AZINDUA BODI YA WADHAMINI YA JKCI, KUIMARISHA UTAWALA NA UENDELEVU WA TAASISI

Posted on: June 12th, 2026

Na Atley Kuni, WAF – Dar es Salaam

Serikali kupitia Waziri wake wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa imezindua rasmi Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), hatua inayolenga kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa kimkakati wa taasisi hiyo muhimu katika utoaji wa huduma za moyo nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Juni 12, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kuanzishwa kwa Bodi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha JKCI inaendelea kukua na kutoa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi kwa viwango vya kimataifa.

Amesema Bodi ya Wadhamini itakuwa chombo muhimu cha ushauri na usimamizi kitakachosaidia taasisi kupanga na kutekeleza mikakati ya muda mrefu, sambamba na kusimamia matumizi bora ya rasilimali kwa manufaa ya wananchi.

Mhe. Mchengerwa amesema kuwa katika kipindi ambacho JKCI imeendelea kupanua huduma zake na kupokea wagonjwa kutoka ndani na nje ya Tanzania, kunahitajika mfumo imara wa uongozi utakaoweza kusimamia ukuaji huo kwa ufanisi na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendelea kuwa na ubora unaohitajika.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Bodi ya Wadhamini pia itakuwa na jukumu la kusaidia kuvutia ushirikiano na uwekezaji kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo, sekta binafsi na taasisi za kimataifa ili kuimarisha uwezo wa JKCI katika huduma, tafiti na mafunzo ya wataalamu wa afya.

Mhe. Mchengerwa amebainisha kuwa kuzinduliwa kwa bodi hiyo kunakuja wakati ambapo JKCI imeanza kutekeleza mipango mikubwa ya maendeleo ikiwemo maandalizi ya huduma za upandikizaji wa moyo, upanuzi wa huduma za uchunguzi wa kisasa na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika sekta ya tiba utalii barani Afrika.

Waziri Mchengerwa amewataka wajumbe wa Bodi ya Wadhamini walioteuliwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo ili kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kuwa kielelezo cha ubora katika huduma za moyo.