Wizara Ya Afya

WATAALAM WA MAABARA WAAHIDI KUINUA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: September 18th, 2026

Na Zakayo Mosha- WAF Mwanza

Wataalam wa Maabara wa Sekta ya Umma na binafsi katika mikoa ya Geita,Singida,Mara, Kagera,Tanga,Kilimanjarona Mwanza walioshiriki katika Mafunzo ya usimamizi wa sampuli (sample management and reporting), wameahidi kuendelea kutoa huduma bora za Afya kwa wananchi.

Akizungumza leo Septemba 18,2026 Jijini Mwanza wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo Bw.James Hellar Afisa Kitengo cha Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya amewaasa Wataalam hao kutumia maarifa na ujuzi waliopata katika kutoa vipimo sahihi na kwa wakati ili visaidie katika utoaji wa maamuzi ya matibabu kwa Wananchi.

Amewasisitiza Wataalam hao kuendelea kushirikiana katika utendaji kazi na kuzingatia miongozo,sheria na taratibu zilizowekwa na Wizara ya Afya katika utayari wa kujikinga na kudhibiti magonjwa ya mlipuko ikiwemo Ebola,Marburg na Mpox yasiingie hapa nchini

Naye mshiriki wa mafunzo hayo Bi.Riziki Chillambo mtaalam wa maabara Hospitali binafsi ya Waja Mkoa wa Geita,kwa niaba ya washiriki wenzake ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya afya kwa kuwashirikisha wataalam wa sekta binafsi katika Mafunzo hayo muhimu.

Amesema mafunzo hayo yamewawezesha kuongeza ujuzi na maarifa mapya ya namna bora na sahihi ya uchukuaji, Uchakataji na usafirisha salama wa sampuli za Magonjwa ya mlipuko ikiwemo Marburg,Mpox na Ebola kwa kuzingatia usalama wa watoa huduma za afya na wananchi.

"Kwa niaba ya Wataalam wenzangu napenda kuiomba Serikali kupitia Wizara ya afya pamoja na Shirika la Afya duniani(WHO) kuendelea kutoa mafunzo kama haya mara kwa mara ili kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya kwa Wananchi" amesema Bi.Riziki

Kwa upande wake Bw. Joakim John Chacha Mratibu wa huduma za Maabara sehemu ya Uchunguzi,Ufuatiliaji, na uthibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya amesema jumla wa washiriki 42 wameshiriki mafunzo hayo kutoka Sekta ya Umma na binafsi