TMDA ISOMANE NA MFUMO WA BIMA YA AFYA NCHINI
Posted on: October 19th, 2026Waziri wa Afya,Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuunganisha mifumo yake ya TEHAMA na mifumo ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuimarisha udhibiti wa dawa na kuunga mkono utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote nchini.
Akizungumza Oktoba 19, 2026, jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Afya kwa TMDA,Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema dawa ambazo hazijasajiliwa na TMDA hazipaswi kulipiwa kupitia bima ya afya, akieleza kuwa hatua hiyo itaongeza nguvu katika mapambano dhidi ya dawa zisizokidhi masharti ya udhibiti.
“Dawa ambayo haijasajiliwa na TMDA isilipwe na bima ya mtu yeyote. Hiyo ni silaha ya ziada katika vita hii,” amesema Mchengerwa.
Vile vile amesisitiza kuwa mifumo hiyo inapaswa kusomana ili kurahisisha uthibitishaji wa usajili wa dawa kabla ya malipo kufanyika, hatua itakayosaidia kuimarisha uwajibikaji katika matumizi ya fedha za bima na kulinda wananchi dhidi ya dawa zisizokidhi viwango vinavyotakiwa.
Hatua hiyo ina umuhimu katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayotambua afya kama msingi wa maendeleo ya uchumi, huku udhibiti madhubuti wa dawa ukiwa muhimu katika kulinda nguvu kazi ya Taifa na kuimarisha mfumo wa huduma za afya.
Mchengerwa ameitaka TMDA kutumia nafasi yake kimkakati kuhakikisha dawa zinazowafikia wananchi zinakidhi viwango vya ubora, usalama na ufanisi, akisisitiza kuwa uwekezaji katika udhibiti wa dawa ni sehemu ya kulinda afya za wananchi na kujenga uchumi imara wa Taifa.