Wizara Ya Afya

TANZANIA YAWEKA SHABAHA MPYA YA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO VITOKANAVYO NA UZAZI

Posted on: September 15th, 2026

Na Abduly Madenge, WAF-MOROGORO

Serikali imeweka shabaha mpya ya kuendeleza mapambano dhidi ya vifo vitokanavyo na uzazi mbali ya mafanikio yaliyopatikana kwa sasa wanalenga kushusha vifo vya mama hadi chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030/31.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Watoto na Vijana katika Idara inayohusika na Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dkt. Felix Bundala, Septemba 12, 2026 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha maandalizi ya mpango kazi wa miaka mitano wa RMNCAH (ONE PLAN IV) kinachofanyika Mkoani Morogoro.

Dkt. Bundala amesema shabaha hiyo imeainishwa katika Mpango Mkakati unaoandaliwa wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31, unaolenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa afua za kupunguza vifo vya mama, watoto wachanga na watoto walio chini ya miaka mitano.

“Tumepiga hatua kubwa, lakini mafanikio hayawezi kuwa mwisho wa safari. Tunapaswa kuongeza kasi ya utekelezaji wa afua ili kufikia shabaha tulizojiwekea na kuhakikisha vifo vinapungua zaidi,” amesema Dkt. Bundala.

Amesema Tanzania imefanikiwa kushusha vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2021/22, hatua ambayo imeweka msingi wa kuendelea kupunguza vifo hivyo.

“Licha ya kushuka kwa kiwango hicho, bado tunahitaji kufanya zaidi kwa sababu 104 ni juu ya matarajio yetu; ndiyo maana tumeweka shabaha ya kufikisha chini ya 70 ifikapo mwaka 2030/31,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Bundala amesema Serikali inalenga kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 24 hadi 12 kwa kila vizazi hai 1,000, huku vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vikilenga kushuka kutoka 43 hadi 25 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2030/31.

Amesema kufikia shabaha hizo kutahitaji tathmini ya kina ya utekelezaji wa mpango uliopita, ikiwemo kubaini mafanikio, changamoto na mapungufu yaliyopo, ili kuainisha afua zenye matokeo makubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.