TANZANIA YAPIGA HATUA SEKTA YA AFYA
Posted on: September 12th, 2024Na WAF - Dar Es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga hatua kubwa katika Sekta ya Afya kwa kudhibiti VVU, TB na Malaria, mifumo ya Afya iliyostahimilivu na endelevu pamoja na kuboresha utendaji wa kazi kwa watumishi.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Septemba 12, 2024 wakati wa kikao cha pamoja na Mkuu wa Idara, High Impact 2 wa Global Fund Bw. Linden Morrison kilichofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar Es Salaam.
"Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa msaada mkubwa wa kifedha na kiufundi unaotolewa na Global Fund, kwa miaka mingi msaada huu umetuwezesha kupata maendeleo makubwa katika kudhibiti VVU, TB na Malaria huku pia tukijenga mifumo ya Afya iliyostahimilivu na endelevu." Amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama amesema kupitia uimarishaji wa afua za kuzuia na kuongezwa kwa huduma na matibabu, maambukizi mapya ya VVU na vifo vinavyohusiana na UKIMWI vimepungua ambapo Tanzania imepata maendeleo makubwa kuelekea malengo ya 95-95-95, ambayo kwa sasa yanasimama katika 83-98-94.
Amesema, kwa sasa mifumo ya Afya imeimarika kwenye vituo vya afya pamoja na mifumo ya Afya ya jamii ambapo Tanzania imejiandaa kukabiliana na magonjwa ya milipuko endapo itatokea nchini.
"Serikali imepiga hatua katika utunzaji wa watoto wachanga kwenye vituo 523 vya huduma ya Dharura ya Uzazi (CEmOC), tunaomba usaidizi wa kuanzisha vitengo vingine zaidi ili tuweze kuokoa maisha ya watoto hao pamoja na usaidizi wa kifedha kwa ajili ya kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwemo wa Mpox." Amesema Waziri Mhagama