TANZANIA YAENDELEA KUONYESHA NJIA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI, KUDHIBITI MAGONJWA YA MLIPUKO
Posted on: August 17th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam
Tanzania imeendelea kuonyesha njia katika juhudi za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga, sambamba na kuimarisha mifumo ya kinga, ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya mlipuko katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema hayo leo Agost 17, 2026 wakati akifungua Mkutano wa Kamati ya Ushauri ya Kitaalam ya Kikanda (ReTAC), unaowakutanisha Makatibu Wakuu, Waganga Wakuu wa Serikali na wataalamu wa afya kutoka nchi 14 wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuelekea Mkutano wa Nne wa Kamati ya Uongozi ya Kikanda ya Mawaziri wa Afya (ReSCO).
"Uzoefu wa Tanzania umeonyesha kuwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga kunahitaji utashi wa kisiasa katika kuwekeza kwenye huduma za dharura, kuongeza bajeti ya afya hususan katika eneo la afya ya uzazi, mama na mtoto, pamoja na kuhakikisha watumishi wa afya wanapatiwa mafunzo na ujuzi wa kutosha ili kutoa huduma bora na za dharura kwa wakati," amesema Dkt. Magembe
Aidha, Dkt. Magembe amesema jambo kubwa ambalo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya na anaendelea kufanya ni kuwa na utashi wa kisiasa na kuhakikisha mikakati inayowekwa inatekelezwa kwa vitendo na siyo kubaki kuwa maneno au miongozo mizuri iliyochapishwa kwenye vitabu na majarida.
Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe amezishukuru nchi wanachama kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania, jambo linalowezesha nchi kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa katika mipaka na maeneo yanayopakana na nchi nyingine.
"Hatua hii kubwa imechangia kuilinda Tanzania dhidi ya magonjwa ya mlipuko yanayoendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo ya ukanda huo," amesema Dkt. Magembe
“Hakuna nchi inayoweza kuwa salama kama nchi nyingine haiko salama, kuna umuhimu mkubwa sana wa nchi za Afrika Mashariki kushirikiana katika kuzuia, kugundua na kudhibiti magonjwa ya mlipuko, ndiyo maana leo tupo hapa kwa lengo la kubadilishana uzoefu huo,” amesema Dkt. Magembe.