Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SIKONGE KUANZA HUDUMA ZA UPASUAJI KUFUATIA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA KUWAJENGEA UWEZO

Posted on: October 8th, 2024

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAIWEZESHA SIKONGE KUANZA UPASUAJI


Na WAF, SIKONGE 


Kambi ya Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia imefanikiwa kuanzisha huduma za upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Sikonge mkoni Tabora, huduma ambayo haikuwepo hapo awali katika hospitali hiyo.


Akiongea Oktoba 08, 2024 Hospitalini hapo Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Catherine  Katisho amesema ujio wa Madaktari Bingwa imekuwa ni neema kwao kwani rufani ambazo zilihitaji upasuaji sasa zitakuwa zikifanyika katika hospitali yao.


"Kwa Mwezi tulikuwa na wastani wa wagonjwa kati ya 25 hadi 30 waliokuwa  wakihitaji huduma ya upasuaji hivyo tulikuwa tunalazimika kuwapa rufani kwenda Hospitali ya mkoa Kitete iliyopo umbali wa takribani kilomita 90", amesema Dkt. Katisho.


Katisho ameongeza kuwa miundombinu mingi iliyopo hospitalini hapo ilishindwa kutumika kutokana na kutokuwa na utaalamu wa kutosha na ujuzi lakini ujio wa kambi hiyo utawasadia watumishi wao kujifunza namna ya kuitumia.


"Watumishi wetu tumewashikiza kwa kila Daktari Bingwa ili wavune ujuzi kwa Mabingwa hawa na wakiondoka wawe wametuachia maarifa", amefafanua Dkt. Katisho


Naye Mwakilishi wa Wizara ya Afya Dkt. Eveline  Maziku ametumia wasaa huo kuwasihi watumishi wanaojengewa uwezo kuzingatia mafunzo wanayopewa na Mabingwa hao.


"Kuwapata Mabingwa kwa wakati mmoja kama hivi sio jambo rahisi, lakini Rais Samia Suluhu Hassan ameweza, hivyo tumieni fursa hii sio kushangaa bali kuhakikisha unakuwa na weledi", amesema Dkt. Evelin.


Kwa Nyakati tofauti Madaktari Mabingwa wa Sikonge na Tabora Manispaa wamesema mbali ya kuwaelekeza kinadharia lakini wamekuwa wakifanya kwa vitendo kama kupita wodini na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa. 


Madaktari Bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan wapo mkoani humo kwa muda wa siku sita kutoa huduma za kibingwa kuanzia Oktoba 07 hadi 13, 2024.