Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAZIDI KUWEKA MAZINGIRA RAFIKI UWEKEZAJI VIWANDA VYA DAWA NA VIFAA TIBA

Posted on: January 16th, 2026

Na WAF- Dar es salaam.

Serikali kupitia Wizara ya Afya imefungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ikiwa na shabaha ya kuongeza uzalishaji wa dawa na vifaa tiba ili nchi iweze kufikia uwezo wa zaidi ya asilimia 60 ifikapo 2030.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa dawa za Binadamu na Mifugo, Dkt. Nyola Mwangwisi kwa niaba ya Mfamasia Mkuu wa Serikali, Januari 15, 2026 wakati wa mahojiano maalum na kituo cha ITV jijini Dar es salaam .

“Kuna wito maalum wa kuwataka wale wote wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya uzalishaji dawa na vifaa tiba Tanzania, wito huu ni kwa wafanya biashara wote, yaani watu binafsi, wageni kutoka nje nchi au ushirikiano wa pamoja,” amesema Dkt. Mwangwisi.

Dkt. Mwangwisi amesema kuwa Januari 19, 2025 Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa ataongoza majadiliano ya pamoja katika ukumbi wa Hyatt Hotel ambapo Serikali itaweka bayana nia yake lakini pia kufahamu changamoto kwa wawekezaji ili kupata ufumbuzi wa pamoja.

Dkt. Mwangwisi amefafanua kuwa kongamano hilo kubwa litafungua milango kwa wawekezaji ambao wanaweza kuleta malighafi lakini pia teknolojia ili kuweza kurahisisha uzalishaji.

“Serikali imetoa nafasi kwa wawekezaji wa nje kuja kushirikiana na wazawa ili kuweza kukuza mtaji wa wazalendo katika eneo hilo la viwanda vya dawa na vifaa tiba" amesema Dkt. Mwangwisi.

Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa toka kuteuliwa kwake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka msukumo wa hali ya juu kwa kuwataka watu mbali mbali kuitika wito wa kuwekeza kwenye viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini ili kupunguza gharama za kuagiza toka nje