SERIKALI, WADAU WAKUTANA KUWEKA AFUA YA MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE
Posted on: May 13th, 2025
Na WAF, ARUSHA
Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele kwa kushirikiana na wadau wa afya nchini imeanza kuweka mikakati na kuandaa mpango thabiti wa kudhibiti na kutokomeza magonjwa hayo.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele Dkt. Clara Mwansasu katika kikao kazi cha siku mbili kinachofanyika Jijini Arusha huku kikihusisha timu za uendeshaji ya mikoa na halmashauri tatu (3) za mkoa wa Arusha ambapo baada kikao hicho kukamilika utekelezaji utafuata.
"Lengo la kikao hiki ni kuja na mpango thabiti utakaotumika kutekeleza afua jumuishi ikilenga kupunguza gharama za utekelezaji wa afua hizi katika ngazi ya jamii ikizingatiwa kuwa kwa sasa vinatumika vyanzo vya ndani kwenye kutekeleza afua hizo," amesema Dkt. Mwansasu.
Aidha Dkt. Mwansasu ameongeza kuwa utekelezaji wa mpango huo ni utekelezaji wa ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa mwaka 2022 alipokuwa akiweka saini azimio la Kigali ambapo waliahidi kuongeza mapato ya ndani katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele.
Wakizungumza kwa niaba ya wadau wengine, mdau kutoka katika shirika la Helen Keller International na Insupply Health Tanzania...........
wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuiwezesha Serikali kuwa na muendelezo katika mipango na mikakati iliyojiwekea na kufikia malengo yake ya kutoka huduma bora kwa wananchi.
Awali wakati wa ufunguzi wa kikao hicho ilielezwa kuwa kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa kichocho na minyoo ya tumbo ni chini ya asilimia 2 kimkoa, kwa mkoa Arusha unatumika kama mkoa wa mfano.
Aidha maambukizi ya ugonjwa wa trakoma yamepungua kwa zaidi ya asilimia 40 tangu program za udhibiti zianze ili hali maambukizi ya ugonjwa wa trakoma yamepungua kutoka asilimia 52.5 hadi asilimia 8.5 Ngorongoro, asilimia 57.6 hadi 14.9 Longido na asilimia 57.6 hadi 9.1 Monduli.