MCHENGERWA: AITAKA TMDA KUIMARISHA UDHIBITI NA KUONGEZA UZALISHAJI WA DAWA NCHINI
Posted on: October 19th, 2026Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Mb), ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuimarisha mifumo ya udhibiti wa dawa ili kusaidia kufanikisha lengo la Serikali la kuzalisha nchini asilimia 80 ya mahitaji ya dawa na bidhaa za afya ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza Oktoba 19, 2026, jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Afya kwa TMDA (MAB), Mhe. Mchengerwa amesema mamlaka imara na inayoaminika ni msingi muhimu wa kuvutia uwekezaji katika viwanda vya dawa na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakubalika katika masoko ya kimataifa.
Amesema TMDA ina jukumu la kuhakikisha kuwa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani zinasajiliwa kwa wakati, bila kuathiri viwango vya ubora na usalama. Aidha, amesisitiza umuhimu wa ukaguzi wa viwanda kufanyika kwa weledi na uadilifu ili kuimarisha imani kwa bidhaa za afya zinazozalishwa hapa nchini.
“Mdhibiti imara ni msingi wa uchumi wa dawa,” amesema Mhe. Mchengerwa, akieleza kuwa umahiri wa TMDA una mchango katika kukuza ajira, kuongeza mapato ya kodi, kuokoa fedha za kigeni na kuimarisha usalama wa Taifa.
Vilevile, amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatambua sekta ya afya kama eneo muhimu katika maendeleo ya uchumi, hivyo TMDA inapaswa kuwa sehemu ya timu ya kitaifa inayotekeleza ajenda ya kuendeleza viwanda vya dawa nchini.
Kutokana na hilo, ameitaka Bodi mpya ya Ushauri ya Wizara ya Afya kwa TMDA kusimamia mikakati itakayoiwezesha Mamlaka hiyo kuendelea kuboresha utendaji wake, kuvutia uwekezaji katika viwanda vya dawa na kuimarisha ushindani wa bidhaa za afya zinazozalishwa nchini.