Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MADAKTARI BINGWA, BINGWA BOBEZI WA RAIS SAMIA WAFIKIA WANANCHI 350 KANDA YA KUSINI MASHARIKI

Posted on: May 7th, 2024



Na WAF - Lindi

Wananchi zaidi ya 350 wamejitokeza na kupatiwa matibabu kwenye Kambi ya Maalumu ya madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wa Rais Samia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi - Sokoine.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa wa wilaya ya halmashauri ya manispaa ya Lindi mhe. Shaibu Ndemanga Leo Tarehe 6, Mei 2024 mara baada ya uzinduzi wa huduma ya mkoba ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi wa Rais Samia, Kanda ya Kusini Mashariki katika hospitali ya rufaa ya Sokoine Mkoani wa Lindi.

Mhe. Ndemanga amesema Ili kuwafikia wananchi wengi Zaidi na kuendelea kuboresha Huduma za Afya, itatolewa huduma bure ya kumuona daktari kwa wagonjwa wasio na bima lakini mgonjwa atatakiwa kuchangia kiasi kidogo iwapo atahitajika kupata huduma zinginezo ikiwemo huduma ya vipimo, dawa na huduma za upasuaji.

“Tunatoa shukrani za dhati kwa Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya utoaji wa Huduma za Afya kwa kwa kupeleka fedha za ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za Afya pamoja na manunuzi ya vifaa tiba” amesema Mhe. Ndemanga

Aidha, Mhe. Ndemanga amewaomba wananchi wote wenye matatizo ya kiafya kuhudhuria ya kwenye kambi hiyo ili kuonana na kutibiwa na madaktari Bingwa na Bingwa bobezi ambapo itasaidia kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu nje ya mkoa huo kufuata huduma.

Kambi ya Matibabu ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wa Rais Samia imeanza leo tarehe 07 Mei na kutarajiwa kumalizika tarehe 10 Mei, 2024 kwa Kanda ya Kusini.