Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

MAADHIMISHO YA KISWAHILI YAGUSA SEKTA YA AFYA

Posted on: July 8th, 2025

Wizara ya Afya imeshiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, kitaifa visiwani Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kutambua na kuongeza uimara wa mawasiliano yake hasa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.


Akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho hayo leo Julai 7, 2025 Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Dkt. Ona Machangu, amesema kiswahili kimekuwa nyenzo muhimu ya kusambaza taarifa za fya na njia ya kutoa huduma za afya nchini.


Amesema, kwa ushirikiano na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) Wizara imekuwa ikitoa taarifa zenye ufasaha wa lugha ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kuongeza tija kwenye sekta ya afya.


“Tumekuwa tukishirikiana na mabaraza haya mawili kwasababu tunatambua wao ndiyo wamepewa jukumu la kuratibu, kwahiyo wakati tukiwa tunaendelea kuandaa maudhui mbalimbali ya uelimishaji, sehemu ya elimu ya afya kwa umma imehakikisha  inashirikiana bega kwa bega ili lugha iwe rahisi kwa mwananchi kuelewa na kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ya mlipuko,” amefafanua Dkt. Machangu.


Naye,  Mwenyekiti wa Baraza ka Kiswahili Tanzania (BAKITA), Prof. Martin Mhando, amesema baraza limejikita  upande wa afya kwa muda mrefu ili kuhakikisha wananchi wanaelewa huduma za afya ikiwemo wanachapisha vipeperushi vinavyobeba maudhui ya afya.


“Kusema ukweli kwa upande wa afya ni upande ambao BAKITA imekuwa ikijikita kwa muda mrefu kwasababu bila maelewano kati ya mtoa huduma wa afya na mgonjwa itakuwa ni changamoto kubwa, hivyo huwa tunashirikiana na wenzetu wa afya ili watoe maelekezo kwa ufanisi mkubwa wa lugha na wananchi wapate huduma bora,”amesema Prof.Mhando.


Dunia huadhimisha siku ya lugha ya kiswahili kila ifikapo Julai 7 ambapo kitaifa maadhimisho hayo yamefanyika visiwani Zanzibar. Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Kiswahili kwa Amani na mshikamano’ ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa  Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdalla, yalihudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa  michezo na  Prof. Palamagamba Kabudi.