IMARISHENI MKAKATI WA KUSIMAMIA USAFI WA MAZINGIRA
Posted on: September 9th, 2024Na WAF - Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema ili kuepuka magonjwa ya mlipuko ameitaka Idara ya Kinga Wizara ya Afya kuimarisha mpango mkakati wa kusimamia suala la usafi wa mazingira katika majiji makubwa pamoja na maeneo ya mipakani mwa nchi.
Waziri Mhagama amesema hayo leo Septemba 9, 2024 wakati wa kikao na Idara ya Kinga Wizara ya Afya kwa lengo la kujadiliana utendaji kazi wa idara hiyo pamoja na kujua majukumu ya Idara hiyo.
"Tukumbushane kuzingatia usafi, kuanzia katika mikoa mikubwa (majiji) kama vile mkoa wa Dodoma, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza pamoja na mipakani hii itaweza kusaidia mikoa mingine kuiga mfano huu na hatamaye tutafanikiwa nchi nzima." Amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama ameelekeza kutengenezwa kwa programu maalum ya kusimamia suala la matumzi ya vyoo bora ambavyo vitatumika kwa ufasaha ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko na kuleta usalama wa Afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kinga Dkt. Ntuli Kapologwe wakati akiwasilisha taarifa yake amesema, Afya ya Mazingira inajumuisha afua zinazolenga kuzuia visababishi vya magonjwa ambapo afua hizo ni pamoja na usafi wa mazingira, udhibiti wa wadudu wadhurifu na wanyama waharibifu.
"Lakini pia afua nyingine ni pamoja na udhibiti wa taka, usalama wa chakula, usalama wa maji ya kunywa, udhibiti wa magonjwa mipakani, huduma za Afya mahala pa kazi pamoja na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira." Amesema Dkt. Ntuli
Idara ya Kinga inajukumu la kuandaa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo ya huduma za Afya Kinga na kusimamia utekelezaji wake, kuandaa na kusimamia utoaji wa elimu na hamasa katika masuala ya Afya kwa umma, kuratibu na kukuza utafiti katika Sekta ya Afya.
Vilevile inajukumu la kuratibu na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Mganga Mkuu wa Serikali kwenye masuala yote yanayohusiana na huduma za Afya kinga nchini, kuratibu usanifu, uendelezaji na usambazaji wa taarifa za Afya Kinga pamoja na nyenzo za mawasiliano nchini.