DAS NYAMAGANA DC AWATAKA VIJANA KUFANYA MAAMUZI SAHIHI KWA MUSTAKABALI WA MAISHA YAO
Posted on: October 31st, 2026Na Atley Kuni, WAF – Mwanza
Bonanza la Jiongeze 360 lililofanyika jijini Mwanza limefanikiwa kuwafikia vijana zaidi ya 4,000 kutoka shule na vyuo mbalimbali, likiwa na lengo la kuwajengea uelewa kuhusu afya ya uzazi, kufanya maamuzi sahihi na kujiandaa kwa maisha bora ya baadaye.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga bonanza hilo, iliyofanyika Oktoba 31, 2026, Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana, Thomas Salala, amewataka wanafunzi kutumia elimu waliyoipata kama msingi wa kujenga maisha yao, kutimiza ndoto na kufikia malengo waliyojiwekea.
Salala amesema kaulimbiu ya bonanza hilo inatoa ujumbe muhimu kwa vijana kuhusu umuhimu wa kujiandaa mapema kwa ajili ya maisha ya baadaye, akisisitiza kuwa mafanikio ya mtu hujengwa kupitia maamuzi anayoyafanya akiwa katika umri mdogo.
Ameeleza kuwa elimu ya afya ya uzazi ni nyenzo muhimu kwa vijana, kwani huwasaidia kujitambua, kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri masomo na maendeleo yao, pamoja na kufanya maamuzi sahihi yenye tija kwa maisha yao.
Aidha, amewataka wanafunzi kutobaki na elimu waliyoipata wao pekee, bali wawe mabalozi wazuri kwa wenzao na wadogo zao kwa kuwafikishia ujumbe kuhusu kujitambua, kujilinda na kupanga maisha yao.
"Watoto mliopo hapa, shauku yetu ni kuwaona mkitimiza ndoto zenu. Msikubali kufanya maamuzi yatakayoharibu maisha yenu ya baadaye. Jitulizeni ili mfikie hatua ya kufanya maamuzi sahihi," amesema Salala.
Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kulitumia bonanza hilo kama fursa ya kujifunza, kujitambua na kuweka malengo yatakayowawezesha kuwa na maisha bora, akisisitiza kuwa elimu waliyoipata haipaswi kuishia katika viwanja vya bonanza, bali iwe sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Vijana kutoka Wizara ya Afya, Gerald Kihwele, amesema bonanza hilo ni sehemu ya mwendelezo wa programu ya Mabonanza ya Jiongeze 360, ambayo imeendelea kuonesha matokeo chanya kwa kuwafikia na kuwaelimisha vijana.
"Awali tulifanya bonanza kama hilo mkoani Ruvuma, katika Wilaya ya Tunduru, ambapo mwitikio ulikuwa mkubwa. Hata hivyo, mwitikio wa hapa Nyamagana umetia fora na kutupa nguv