Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ZAIDI YA HUDUMA 35 ZA KIBOBEZI ZINAPATIKANA MUHIMBILI

Posted on: September 10th, 2024

Na WAF - Dar Es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha upatikanaji wa huduma za Ubingwa Bobezi zaidi ya 35 katika Hospitali ya Taifa Muhimbilli (Mloganzira na Upanga) ambazo zimewezeha kupunguza rufaa nje ya nchi. 


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Septemba 10, 2024 akiwa katika Ziara yake ya siku Tatu Mkoani Dar Es Salaam ambapo ameanza kwa kutembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (Mloganzila na Upanga) akiambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Ndg. Ismail Rumatila Na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Dkt. Hamad Nyembea. 


Waziri Mhagama amesema miongoni mwa huduma hizo za Kibingwa ni pamoja na upandikizaji wa Figo kwa njia ya matundu, upandikizaji wa Uloto, uchaguzi na matibabu ya Magonjwa ya Moyo, upandikizaji wa Nyonga na Magoti, kuvunja mawe kwenye Figo kwa kutumia mawimbi mtetemo pamoja na kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kwa kupitia matundu ya pua. 


Amesema, kwa sasa Hospitali zote za Rufaa za Mikoa ukienda kupata huduma za Afya, utapata huduma za kibingwa za aina zisizopungua Nane ambapo katika Hospitali za Taifa kuna aina za matibabu ya Ubingwa Bobezi sio chini ya aina 35. 


"Kwakweli Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi yake kubwa kwa kutujengea majengo, kutununua vifaa na vifaa tiba katika miaka hii Mitatu, Sekta ya Afya imekua sana nchini hasa katika huduma hizi za ubobezi, sasa jukumu ni la kwetu sisi watumishi kuwahudumia Watanzania kwa kuwapa huduma bora." Amesema Waziri Mhagama


Aidha, Waziri Mhagama amesema Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya inaendelea na juhudi za kuifanya kuwa kituo cha utalii wa tiba, tuweze kupokea wageni (wagonjwa) wengi kutoka nje kama Mataifa mengine yanavyopokea wagonjwa kutoka nchi nyingine. 


"Lakini eneo jingine tutakalolipa kipaumbele ni Bima ya Afya kwa wote, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa ya kutengeneza mfumo mzuri wa kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa na huduma za Afya kupitia Bima ya Afya kwa Wote kutoka kwenye Afya Msingi mpaka Hospitali za Taifa ili kuhakikisha mfuko huo unakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa wote." Amesema Waziri Mhagama


Mwisho, Waziri Mhagama amesema ameridhishwa na huduma za Afya ya uzazi kwa akina mama hasa wakina mama wanaojifungua watoto wenye uzito mdogo (njiti) zinazotolewa katika Hospitali hiyo ambalo ndio eneo la msingi la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupunguza vifo vya akina mama na watoto