WIZARA YA AFYA YATAMBULIWA KWA USIMAMIZI MAHIRI WA TAASISI ZAKE
Posted on: August 24th, 2025
Na WAF – Arusha
Ofisi ya Msajili wa Hazina imeipongeza Wizara ya Afya kwa usimamizi bora wa taasisi zake na kupewa tuzo, hatua iliyochangia maendeleo makubwa katika utoaji wa huduma, matumizi sahihi ya rasilimali na ufanisi wa kiutendaji.
Pongezi hizo zimetolewa na Msajili wa Hazina, Bw. Nehemia Mchechu, Agosti 24, 2025, wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs Forum 2025) kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Katika Kikao kazi hicho, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ndiye aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Bw. Mchechu amezitaja taasisi hizo kuwa ni Bohari ya Dawa ya Taifa (MSD), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), ambazo zimeelezwa kuwa zimekuwa na mikakati thabiti ya kusimamia rasilimali, kuimarisha mifumo ya utoaji huduma na kuongeza ubora wa huduma za afya nchini.
Pongezi hizo ziliambatana na tuzo ambayo ilipokelewa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe kwa niaba ya Wizara ya Afya.
Katika utoaji wa tuzo hizo JKCI imeshinda nafasi ya kwanza katika kipengele cha uboreshaji wa utoaji huduma, tuzo iliyopokelewa na Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Dkt. Peter Kisenge huku TMDA imechukua nafasi ya pili katika kipengele cha Utawala Bora na Uwazi.
MSD imetangazwa kuwa Mshindi wa Pili katika kipengele cha taasisi zinazofanya biashara kwa ufanisi, kwa kuzingatia matumizi, mapato na rejesho la mtaji. Tuzo hiyo imepokelewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa MSD, Bi. Rosemarry Silaa, akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa MSD, Bw. Mavere Tukai.
Ushindi wa MSD umetajwa kuwa kielelezo cha hatua kubwa zinazochukuliwa na Bohari ya Dawa katika kuboresha mifumo ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vifaa vya maabara nchini, sambamba na kuhakikisha uendelevu wa biashara kwa manufaa ya wananchi.
Wizara ya Afya imeendelea kuonyesha mfano dhabiti wa utendaji na uwajibikaji, hali inayochochea utoaji bora wa huduma za afya, upatikanaji wa da