WIZARA YA AFYA YAPOKEA VIDONGE MILIONI MBILI KUKABILIANA NA MINYOO KWA WATOTO
Posted on: August 23rd, 2025
Wizara ya Afya imepokea msaada wa vidonge milioni mbili vya Albendazole venye thamani ya Shilingi Milioni 552 ambavyo ni muhimu katika kuzuia minyoo ya tumbo ambayo huathiri kwa kiasi kikubwa lishe,ukuaji na utambuzi wa watoto chini ya miaka mitano.
Msaada huo uliotolewa na Shirika la World Vision kwa Wizara ya Afya kupitia Idara ya huduma za dawa ni ushahidi wa dhamira thabiti wa Serikali ya kuboresha afya ya umma hususan afya ya mtoto kupitia kampeini zake za Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto zinazofanyika mwezi Juni na Disemba kila mwaka.
Mwakilishi wa Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw.Abdalla Mushi akizungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea dawa hizo amesema pamoja na umuhimu wa Albendazole, msaada huo umekuja wakati muhimu Serikali inapofanya maandalizi ya kampeini za mwezi wa afya ya lishe ya mtoto inayohusisha utoaji wa vitamini A, dawa za kutibu minyoo ya tumbo na kufanya tathimini ya lishe kwa watoto wenye umri wa miezi sita (6) hadi 59 itakayofanyika Disemba mwaka huu nchini.
Naye Mkurugenzi mwandamizi wa Shirika la World Vision Tanzania anayeshughulikia mahusiano ya Shirika lake na Serikali Dkt. Joseph Mitinje amepongeza juhudi za Serikali za kutambua kuwa taifa endelevu ni lile linalohudumia watoto na kuweka kipaumbele katika kuwahudumia kiafya.
Aidha Dkt. Mitinje ameongeza kuwa Shirika la World Vision, Bohari Kuu ya Dawa, Wizara na Mashirika kwa muda sasa wameshirikiana kuhakikisha wanapambana kuondoa minyoo katika miili ya watoto akibainisha kuwa mwaka huu Shirika linaendeleza utamaduni huo wa kuchangia dawa za Albendazole.
Wakati huohuo Mratibu wa zoezi la Kampeini ya Mwezi wa Afya na Lishe kutoka Wizara ya Afya Bw. Peter Kaswahili amesema Wizara ya Afya iko katika maandalizi ya kampeini hiyo kwa mwezi Disemba hivyo anatoa shukurani zake kwa Shirika la World Vision kwa kuchangia katika afya ya ustawi wa watoto hapa nchini.