WIZARA YA AFYA, EXIM BANK WAJADILI MASHIRIKIANO KATIKA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: March 25th, 2025
Na WAF - Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amekutana na ujumbe kutoka Exim Bank nchini Tanzania kwa lengo la kujadiliana namna bora ya kuendeleza mashirikiano na Wizara ya Afya ikiwemo ya uboreshaji wa huduma za mama na mtoto kwa kufuata taratibu na mifumo ya Serikali.
Waziri Mhagama amekutana na ujumbe huo leo Aprili 11, 2025 katika ofisi za Wizara ya Afya mkoani Dodoma ulioongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Exim Bank Bw. Jaffari Matundu.
"Tuhesabie hiki ni kikao chetu cha kwanza na sasa tuanze hatua za mwanzo na leo tumejadiliana vizuri, hivyo tuendelee kutekeleza yale matakwa ya Serikali na sisi tunawakaribisha sana mrudi nyumbani ili kwa pamoja tuweze kuwahudumia wananchi wetu," amesema Waziri Mhagama.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Exim Bank Bw. Jaffari Matundu amemshukuru Waziri wa Afya pamoja na kuupongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa kuwapa ushirikiano ambapo ameahidi kutekeleza maelekezo yote ya Serikali pamoja na mifumo iliyowekwa ili kwa pamoja waweze kuwahudumia wananchi.
"Mhe. Waziri kwakweli tunakushuru sana lakini pia, sisi kama uongozi wa Exim Bank tayari tumeshajiunga na mifumo ya Serikali na tupo tayari kushirikiana kwa pamoja ili kutoa huduma bora kwa wananchi, tunaomba kupewa miongozo zaidi na tutaitekeleza ili kwa pamoja taweze kuwasaidia wananchi katika huduma za afya," amesema Bw. Matundu.