Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAUZA MIWANI WASIO NA SIFA NJOMBE, IRINGA WAAHIDI KUTOKUUZA FREMU NA MIWANI TIBA

Posted on: August 22nd, 2025

Na WAF, Iringa


Wafanyabiashara katika mikoa ya Iringa na Njombe wameahidi kutokujihusisha na biashara ya miwani tiba mara baada yakupatiwa elimu na Baraza la Optometria.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti Agosti 22, 2025 wamesema walikuwa wakijihusisha na biashara hiyo ya uuzaji miwani tiba kwa wananchi bila kujua ni kosa kisheria kulingana na miongozo ya Wizara ya Afya. 


Bi. Tumaini Malya mfanyabiashara katika eneo la Mashine Tatu mjini Iringa, amesema amekuwa akifanya biashara hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu (3) lakini alikuwa hajui kama anatenda kosa.


"Wanapokuja wateja wanakutajia namba ya miwani yake na anaweza kukwambia nahitaji plus one point five, (+1.5), naangalia kwenye hifadhi yangu nampatia. Lakini wengine wanaokuja ni wenye vyeti vinavyoonesha namba za vipimo kutoka vituo vya macho na hospitali, wananitajia mahitaji yao na mimi nawapatia," amesema  Bi. Malya


Kwa upande wao Bw. Ben Misunza na Bw. Ahmed Ally wafanyabiashara ndogondogo katika eneo la Miyomboni mjini Iringa, wamedai hiyo imekuwa ni biashara inayowapatia faida bila kutambua kuwa wanaharibu macho ya wananchi.


Awali jopo la Usimamizi Shirikishi likiongozwa na Msajili wa Baraza la Optometria nchini Bw. Sebastiano Millanzi waliwaambia wafanyabishara hao kuwa, ili kujihusisha na biashara ya miwani tiba na vifaa tiba vingine vya optometria sharti awe mtaalam aliyesomea na kusajiliwa na Baraza la Optometria nchini.  


"Kwa kuendelea kufanya biashara hii bila kuwa na utaalam ni kuweka rehani afya za wananchi, hivyo basi kama unataka kuendelea na biashara hii, fuata taratibu zote kwa mujibu wa Sheria ya Optometria Sura ya 23," ameeleza.


  Ameisitiza kuwa ni muhimu kuacha maramoja uuzaji wa miwani hiyo na kuwa mabalozi wa kuwaelimisha wengine. 


Naye Bw.

 Kalidushi Kubingwa Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, akizungumza kwa nyakati tofauti mkoani Njombe na Iringa alizihimiza Timu za Usimamizi za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha zinawasaidia wafanyabiashara hao kufuata taratibu.


"Tunapita kuwapa elimu ninyi mnaotoa huduma ya macho hususani huduma za Optometria, lakini jukumu hili linabaki kwa mikoa na halmashauri kuwasaidia na kuwasimamia katika maeneo yao kuhakikisha linakuwa zoezi endelevu" amesema Bw. Kubingwa.


Zaidi vituo 35 vinavyojishughulisha na shughuli za Optometria kwa mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Iringa vimepatiwa elimu, ushauri sambamba na vingine kupewa wiki moja (1) mpaka miezi mitatu (3) kuboresha maeneo yao ya utoaji huduma.