Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATUMISHI WIZARA YA AFYA WAPEWA MAFUNZO, MBINU KUKABILIANA NA MOTO

Posted on: August 11th, 2025

Na WAF, Dodoma.


Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Afya wamepata mafunzo juu ya aina mbalimbali za vyanzo vya moto na  mbinu za uzimaji wa moto ikiwemo  namna ya kuepuka ajali za moto.


Mafunzo hayo yametolewa kwa watumishi kutoka kwa jeshi la uokoaji na uzimaji moto yakilenga kuwajengea uwezo kukabiliana na dharura mbalimbali zitokanazo naajanga ya moto.


Mafunzo hayo yametolewa  Agosti 11, 2025 Ofisi ya Wizara ya Afya, makao makuu, Mtumba na Mrakibu msaidizi wa Jeshi la Uokoaji na uzimamoto Bw. Stephen Katte ambaye ni Afisa Habari, uhusiano, mawasiliano na elimu kwa Umma wa jeshi hilo.


Akizungumza mara baada ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo, Mkurugenzi msaidizi wa huduma za uuguzi na ukunga,  Bw. Paulo Magessa amesema mafunzo hayo  kwa watumishi wa umma ni ya manufaa kwakuwa elimu hiyo imefungua uelewa juu ya viashiria vya moto na namna ya kutumia vifaa vya moto kujilinda.


‘’Baada ya mafunzo haya watumishi tunapaswa kuchukua hatua kabla ya jambo halijawa kubwa, kufahamu matumizi sahihi ya mitungi na kuzingatia alama za moto na nini kifanyike.


Kwa upande wake Afisa Tawala Mkuu wizara ya Afya Bi. Vivian Boniface akizungumza wakati wa semina hiyo  amesema mafunzo hayo yamemsaidia kujua namna gani ya kuepuka athari za moto na sio tu kwa ofisini bali hata 

nyumbani na mazingira mengine ya viashiria vya moto.


“Kwakweli mafunzo haya yaliyotolewa na Jeshi la Uokoaji na Uzimaji Moto yamenisaidia kujua kwamba ni upande gani nisimame wakati wa kuzima moto na vitu gani vya kuzingatia na kuepuka hapa ofisini lakini pia hata majumbani," amesema  Bi. Vivian.


Awali akitoa mafunzo hayo  Bw. Katte aliweka bayana viashiria na namna ya kudhibiti moto pamoja na jinsi ya kupata msaada wa zima moto. 


“Tupo hapa Wizara ya Afya kwa lengo la kuendeleza majukumu yetu ya kutoa elimu juu ya kuchukua tahadhari za majanga ya moto kwa lengo la kupunguza au kuondoa kabisa majanga hasa ya moto yasiweze kutokea,” amesema.


Katika semina hiyo ya elimu ya janga la moto watumishi wa Wizara ya Afya ambavyo wameonesha kufurahishwa huku wakiahidi kuwa mabalozi kwa jamii zao.