Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATOTO WANAONYONYA MAZIWA YA MAMA WAFIKIA KIWANGO CHA 64%.

Posted on: August 7th, 2025

Na. WAF, Dodoma


Wizara ya Afya imesema watoto wanaonyonya maziwa ya mama kwa sasa ni 64% ya watoto wanaonyeshwa  kwa takwimu za mwaka 2024 hali inayomotisha  jamii na wadau kumlinda mtoto dhidi ya magonjwa mbalimbali yatokanayo na ukosefu wa kinga bora inayopatikana kwenye maziwa ya mama.


Akiongea wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Unyoshaji leo Agosti 7, 2025 Jijini Dodoma Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe Wizara ya Afya Bi.Neema Joshua amesema kwa kipindi cha miaka 30 takwimu hazikuwa nzuri hivyo mafanikio ya sasa ni jitihada kubwa za serikali na wadau mbalimbali wa afya.


“Tumetoka mbali na hali haikuwa nzuri tangu miaka ya 1992, lakini sasa angalau tunakoelekea panaleta mwanga mkubwa ndiyo maana leo kwenye hili tamasha la mpira kwa vijana, tumewahusisha hawa vijana kwasababu bado ni wadogo waweze kujua umuhimu wa unyosheshaji maziwa ya mama kwa mtoto kwa afya za watoto lakini pia kwa ukuaji na maendeleo ya watoto, leo wanacheza mpira lakini tunaamini hawa ndiyo watakuwa akina baba, na wengine tayari ni akina baba kwenye hizi timu,” – amesema Bi Neema.


Naye Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni mratibu wa Maadhimisho hayo Bi. Erieth Rumanyika amesema idadi kubwa ya maafisa wa ngazi mbalimbali kutoka serikalini imetumika kuhakikisha elimu ya unyonyeshaji inawafikia wananchi kwa ufasaha ili kuleta tija kwenye maadhimisho hayo.


“Maafisa wetu wametoa uhamasishaji kupia redio, majukwaa mbalimbali ya kijamii na yote ni kuhakikisha jamii inapata uelewa wa umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama lakini kwa pamoja tuweze kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji wa maziwa ya mama,” amesema Rumanyika


Kwa upande wake Isihaka Maguzi ambaye ni mdau aliyejitokeza kushiriki kilele cha maadhimisho hayo, amewasihi akina baba kushiriki kwenye hatua za muhimu kwa mama mjamzito mpaka anapojifungua ili kupata elimu ya msingi kuhusu afya ya mtoto na namna bora ya kunyonya.