Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATANZANIA TUONGEZE BIDII MAPAMBANO DHIDI YA MALARIA

Posted on: April 26th, 2025

Na WAF, DODOMA

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameitaka jamii ya Watanzania kuongeza jitihada kwenye vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria ili kufikia malengo ya millenia ya kukabili ugonjwa huo ifikapo 2030.

Mhe. Mhagama ametoa kauli hiyo Aprili 25, 2025 jijini Dodoma mbele ya waandishi wa habari alipokuwa akitoa tamko la siku ya malaria Duniani ambapo amesema Tanzania imeendelea kupiga hatua katika mapambano hayo.

"Kiwango cha maambukizi kimepungua kwa asilimia 40 kutoka asilimia 14 hadi 8.1 kwa mwaka 2022 hali inayotia matumaini kwenye safari ya kuutokomeza ugonjwa huu," amesema Mhe. Mhagama.

Mhe. Mhagama ameongeza kuwa, mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma na Iringa imeendelea kuzingatia afua za malaria na hivyo kuwa chini ya asilimia moja cha maambukizi ya Malaria.

Mhe. Mhagama ameutaja mikoa wa Tabora kuwa na kiwango cha juu cha asilimia 23, Mtwara asilimia 20, Kagera asilimia 18,Shinyanga asilimia 16, na Mara asilimia 15 amesema mikoa husika ina kila sababu ya kuongeza juhudi za makusudi ili kushusha na kwenda sambamba na jitihada za Serikali.

"Chini ya Uongozi wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeriďhia kutoa kiasi cha Bilioni 10 kwa ajili ya dawa za kunyunyiza na kuua mazalia ya mbu kwa Halmashauri zote 184," amesema Mhe. Mhagama.

Waziri Mhagama ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi kwenye ngazi zote kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI, kutoa ushirikiano wa kutosha ili dhamira ya Mhe. Rais ya kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika kwa kutokuruhusu Mazalia ya Mbu.

Mhe. Mhagama ameonya matumizi yasiyo rasmi ya Chandarua kwani imekuwa ikichochea kukwamisha jitihada za Serikali kwenye mapambano huku akiwaasa wananchi kuwahi kwenye vituo vya kupimwa kwani sio kila homa ni Malaria.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Malaria kwa mwaka 2025 ni Malaria Inatokomezwa na Sisi: Wekeza, Chukua Hatua - Ziro Malaria Inaanza na Mimi”