Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATAALAMU WAKUTANA KONGAMANO LA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: October 29th, 2024

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu leo Oktoba 29, 2024 ameshiriki kwenye Kongamano la Bima ya Afya kwa wote na Jukwaa la Kimataifa la Ugharamiaji wa Huduma za Afya katika Sekta ya Afya, linalofanyika katika Mkoa wa Arusha.

Kongamano hilo la kwanza kuhusu Bima ya Afya kwa wote linawakutanisha kwa pamoja Wataalamu na wadau Sekta ya Afya katika kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya Mwaka 2023.

Akiwa katika kongamano hilo, Prof. Nagu amesema kuwa lengo la Wataalam pamoja na wadau hao kukutana ni kupeana uzoefu na kupata taarifa za hatua zilizofikiwa pamoja na kuweka mikakati ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

“Serikali inatambua umuhimu wa Bima ya Afya kwa wananchi na tayari imeanza kutekeleza kwa hatua sheria hii ya Bima ya Afya kwa Wote, Kongamano hili litatusaidia kupata uzoefu kutoka maeneo mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi,” amesema Prof. Nagu.

Kongamano hilo la siku nne linalokutanisha kwa pamoja watalaamu, watunga sera, watafiti wa masuala ya afya pamoja na wadau wengine wa sekta ya afya katika kujadiliana namna bora ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote linatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 30 Oktoba, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Arusha(AICC).