Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATAALAMU WA AFYA KATAVI ZINGATIENI WELEDI NA MAADILI YA KAZI; WAZIRI UMMY MWALIMU

Posted on: February 23rd, 2023


Rai imetolewa kwa wataalamu wa afya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi, maadili na viapo vya kazi ili wananchi waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi mara baaada ya kukagua maendeleo ya ujenzi na utoaji huduma katika hospitali hiyo.

“Kazi ya kutoa huduma ya afya ni kazi inayohitaji upendo na utu katika kuhudumia wananchi hivyo natarajia wananchi wa Mkoa wa Katavi watapata huduma bora sambamba na majengo haya mazuri ili kuwa mabalozi wa watumishi wa hospitali hiyo kwa huduma wanazo zitoa kwa wananchi hao” amesema Waziri Ummy.

Ameeleza kuwa akija Mgonjwa lazima asikilizwe, achukuliwe historia yake, vipimo kulingana na historia yake, kuongea na mgonjwa kwa kutumia kauli nzuri na kwa kufanya hivyo kila mtu atakuwa ametimza wajibu wake katika kuhudumia wananchi.

“Wanakatavi wameteseka sana kupata matibabu ya kibingwa kwa kusafiri mwendo mrefu kufata huduma za kibingwa mikoani, hivyo sasa ni wakati wa kuwaonyesha kuwa huduma za kibingwa sasa zinapatikana karibu yao na hakuna haja ya kusafiri kufata huduma hizo kwingine”, amesisitiza Waziri Ummy.

Hata hivyo amesema kuwa madaktari bingwa na wasaidizi wao katika kuhudumia wagojwa wanawajibu wa kupata asilimia ya mapato ya hospitali hiyo ili kuwatia moyo wa kuendelea kufanya kazi

Lakini pia amewakumbusha watumishi hao kuwa serikali ni moja hivyo wnatakiwa kushirikiana na watumishi wa hospitali za Halmashauri katika kutoa huduma ili kuleta ufanisi wa kazi katika mkoa huo.

Waziri Ummy ameelekeza watumishi wa afya wa hospitali hiyo kuwa na utamaduni wa kuwajengea uwezo watumishi wa hospitali za halmashauri katika mkoa huo na watumishi wa halmashauri kuwajengea uwezo watumishi katika vituo vya Afya na Zahanati ili kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma za afya nchini.

Vile vile amesema kuwa mapato yanayopatikana NHIF yatumike kununua dawa na vifaa tiba bila kusahau kuwapa motisha watumishi wa afya ili kuendelea kufanya kazi vizuri

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Onesmo Buswelu ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika amesema kuwa watahakikisha wanatunza miundombinu na vifaa katika hospitali hiyo ili kuendelea kutoa huduma kama ilivyokusudiwa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan

MWISHO