Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI ZAIDI YA 400 KUFANYIWA UPASUAJI WA MTOTO WA JICHO KYELA

Posted on: October 30th, 2024

Na WAF - Mbeya

Watu zaidi ya 400 wenye matatizo ya mtoto wa jicho wanatarajiwa kupatiwa matibabu ikiwemo upasuaji wa mtoto wa jicho wakati wa kambi ya siku tano ya Madaktari wa macho inayofanyika Hospitali ya Wilaya ya Kyela kuanzia Oktoba 30 hadi Novemba 04, 2024.

Hayo yamesemwa Oktoba 30, 2024 na Katibu Tawala wa Halmashauri ya Kyela, Bi. Sabrina Humoud, wakati akizindua rasmi kambi ya matibabu ya macho wilayani humo iliyoratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Helen Keller.

Bi. Sabrina amesema huduma hiyo inalenga kuwasaidia wananchi wenye uhitaji ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu, kwani wataweza kupatiwa huduma hizo bure kupitia mradi wa upasuaji wa mtoto wa jicho.

Aidha, Bi. Sabrina amesema kuhusu umuhimu wa mradi huo ni pamoja na kuwajengea uwezo wauguzi na wataalamu wa Hospitali ya Wilaya ya Kyela, ambao watashiriki wkati wote wa zoezi.

Ametoa wito kwa wananchi wote wenye tatizo la mtoto wa jicho au viashiria vya tatizo hilo kujitokeza ili kupata huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho bila malipo, kwa ajili ya kuwanusuru na ulemavu wa kutokuona.

Kwa upande wake, Mratibu kutoka Mpango wa Taifa wa Macho, Wizara ya Afya Dkt. Greater Mande, amesema ulemavu wa kutokuona haukubaliki, kwani kuna njia za kuzuia na kutibu zikiwemo huduma za gharama nafuu. Amewasihi wakazi wa Kyela kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Helen Keller, Dkt. George Kabona, amesema shirika hilo linawatumia wahudumu wa ngazi ya afya ya jamii kuwashawishi wananchi wenye matatizo kwa njia ya nyumba kwa nyumba, ili kuwafikisha kwenye vituo vya huduma kwa ajili ya upasuaji.