WANANCHI WANUFAIKA NA HUDUMA ZA AFYA KUPITIA WADAU, SERIKALI
Posted on: April 10th, 2025
Na. WAF - Dar es Salaam
Serikali pamoja na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Afya wanaendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya ikiwemo kuimarisha mifumo ya kisekta ambayo inawasaidia wananchi kupata huduma bora za afya na kwa haraka.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Aprili 10, 2025 kwenye maadhimisho ya siku ya afya Duniani yaliyofanyika katika ofisi za Shirika la Afya Duniani (WHO) jijini Dar es Salaam, ambayo yamewakutanisha wadau wa Sekta ya Afya pamoja na sekta binafsi.
"Kwenye maeneo ambayo ni kipaumbele cha Sekta ya Afya tutaendelea kuyafanyia kazi kwa pamoja ikiwemo kuhakikisha watoto wanapata lishe bora kuanzia wanapozaliwa hadi wanapolelewa pamoja na suala la afya ya uzazi kwa ujumla wake kwa sababu suala hili ni jambo la msingi katika uhai wa binadamu," amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amesema tuzo ambayo ameipata Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka nchini Marekani imetolewa baada ya Tanzania kufanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi huku Shirika la Afya Duniani likiitaka Tanzania kupunguza vifo hivyo ifikapo mwaka 2030 hadi kufikia vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ambapo kwa sasa Tanzania ina vifo 104 kutoka vifo 556.
Pia, Waziri Mhagama amesema katika kufanikisha jambo hilo Serikali imeamua kuanzisha Mfuko wa Bima ya Afya kwa wote pamoja na kuweka mifumo ambayo itaweza kuwalipia wale ambao hawawezi kulipia bima hiyo.
"Tunaomba sana wadau wetu kuunga mkono jambo hili ili kuwafikia wananchi wote katika suala la huduma za afya bila ya kuwa na kikwazo cha fedha pamoja na kuhakikisha tunapambana na magonjwa yasiyoambukiza, yanayoambukiza na magonjwa ya mlipuko," amesema Waziri Mhagama.
Katika hatua nyingine, Waziri Mhagama amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha inatengeneza mifumo ambayo itasaidia kufuatilia kwa karibu suala zima la afya katika nchi ya Tanzania, kusomesha madaktari wa ubingwa na ubobezi, kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili kuhakikisha afya za wananchi zinaimarika.