WANANCHI DAR ES SALAAM WAVUTIWA NA HUDUMA YA UPASUAJI WA MABUSHA BILA MALIPO.
Posted on: January 8th, 2026Na WAF, Dar es Salaam
Wananchi mkoani Dar es Salaam waliojitokeza kwenye kambi maalum ya upasuaji Mabusha na Matende wameipongeza Serikali kwa kuliona tatizo hilo na kuandaa kambi maalum ambayo imekuwa msaada kwao.
Wakizungumza katika kituo cha Afya Kinondoni na Kilakala baadhi ya wananchi hao ambao majina yao yamehifadhiwa wamesema huduma hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwao huku wakitoa wito kwa wananchi wengine wenye changamoto ya Mabusha kuchangamkia fursa hiyo ili kupatiwa matubabu.
"Nimehudumiwa vizuri, nashauri na wengine waje wapate huduma hii bila malipo na ninaishukuru sana Serikali" amesema mmoja wa wananchi hao aliyekuwa akikabiliwa na changamoto ya Busha.
Kwa upande wake Dkt. Clara Mwansasu Meneja Mpango wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele kutoka Wizara ya Afya amesema Kambi hiyo ya Upasuaji wa Mabusha itadumu hadi tarehe 30 , Januari, 2026 kwa mkoa wa Dar es Salaam huku akiiasa jamii kuacha unyanyapaa kwa wanajamii wenye changamoto ya maradhi hayo.
Dkt. Aloyce Marenge kutoka Kituo cha Afya Kinondoni amesema kambi hiyo imekuwa na manufaa kwani mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa katika Kampeni hiyo ya Upasuaji wa Mabusha Kituoni hapo.
Zaidi ya Wananchi 500 wanatarajia kufanyiwa upasuaji wa Mabusha Mkoa wa Dar es Salam, huduma iliyoanza kutolewa Januari 5, 2026 na kutarajiwa kutamatika Januari 30, 2026.