Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI 3242 WAJITOKEZA KAMBI YA KIBINGWA MADAKTARI RAIS DKT. SAMIA KANDA YA KATI

Posted on: May 9th, 2025

Na WAF - SINGIDA

Kambi ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia Kanda ya Kati imewafikia wananchi 3,242 na kuwapatia huduma katika maeneo mbalimbali ya kibingwa

Hayo yamebainisha na Ripoti ya kambi hiyo inayohitimishwa leo Mei 9, 2025 mkoani Singida, iliyosomwa na Mwenyekiti wa Kambi hiyo Dkt. Amani Malima ambayo ameeleza kuwa zoezi hilo lililoanza rasmi Mei 05, 2025 hadi kufikia leo, jumla ya kati yao, 1,438 walihudumiwa kupitia NHIF, 942 walilipia papo kwa papo, 73 kupitia bima nyingine na 26 walihudumiwa kwa msamaha.

Kwa upande wa vipimo ripoti hiyo imebainisha jumla ya vipimo 761 vya radiolojia vimefanyika kwa muda wa siku 5 za kambi hiyo huku X- Ray zikiwa 287, USS - 264, ECHO - 91, ECG- 68, CT scan - 47, na vipimo vingine vitano (5).

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Bi. Fatma Mganga akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo amesema kambi hiyo ilikuwa na tija kubwa kwani imewagusa wananchi wa Tanzania.

“Kupitia kazi yenu hii tumewagusa wananchi, wana Singida na Watanzania wenzetu ambao yawezekana walitaabika kwa muda mrefu, wengine kwa kukosa nauli na wengine kukosa nafasi ambao kupitia ninyi mmerudisha faraja na afya miongoni mwao,”.
amesema Bi. Mganga.

Kambi ya Madaktari Bingwa kwa Kanda ya Kati imefanyika mkoani Singida kuanzia Mei 5, 2025 na imefanyika kwa mafanikio makubwa huku baadhi ya wananchi wakipendekeza kuongeza siku ili watu wengi zaidi waweze kufikiwa na huduma hiyo