WANANCHI 150 WAFIKIWA NA HUDUMA ZA KIBINGWA NDANI YA SAA 48.
Posted on: May 29th, 2024
Na. WAF – Mtwara
Wananchi zaidi ya 150 wa Wilaya ya Nanyamba Mkoani Mtwara, wamepatiwa huduma za matibabu ya kibingwa na madaktari bingwa wa Rais Samia katika siku mbili za mwazo wa kambi wa madaktari hao.
Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nanyamba Dkt. Suleiman Kasununu Mei 28, 2024 ambapo amesema wananchi wa wilaya hiyo na maeneo ya jirani wamejitokeza kwa wingi kwa ajili ya kunufaika na huduma za matibabu za kibingwa za madaktari bingwa wa Rais Samia.
Dkt. Kasununu ameongeza kuwa uwepo wa madaktari bingwa hao katika hospitali ya wilaya ya Nanyamba italeta tija kwa madaktari na watumishi wa hospitali hiyo kwa kujengewa uwezo katika maeneo mbalimbali jambo ambalo litachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
“Tunamshukuru madaktari wa bingwa hao kwa ushirikiano wanaoutoa kwa madaktari na watumishi wa hospitali hiyo kwa kuwapatia mafunzo katika maeneo mbalimbali, sisi kama hospitali kwa ujumla wake tutajifunza kutoka kwao na vile vile itatusaidia kuboresha kwenye baadhi ya maeneo ili baada ya kambi hii kuisha basi yale watakayotuachia na sisi tuendelee kuyatekeleza ili kuzidi kuboresha huduma” amesema Dkt. Kasununu.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka hospitali ya rufaa Mkoa wa Pwani- Tumbi Dkt. Adam Gembe amesema muitikio wa wananchi kuja kupatiwa matibabu kwenye kambi ya hiyo ni mkubwa ambapo wagonjwa wengi wanaokwenda kuwaona madaktari ni wale wenye shinikizo la juu la damu pamoja na sukari, na kuongezeka kuwa wamekuwa wakishirikiana na madaktari wa ndani kwa kupeana ujuzi na kufundishana lengo likiwa ni kuwajengea uwezo ili kuzidi kuendelea kuwahudumia wananchi .
Bi. Zuhura Rashidi Asali ni mkazi wa Wilaya ya Tandahimba kutoka kijiji cha Mtama II amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwafikishia huduma hizo za kibingwa karibu na maeneo yao kwa kuwaletea madaktari bingwa wilayani mwao jambo ambalo linawarahisishia kupunguza gharama za matibabu.
Mwisho.