Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANAFUNZI ZUZU SEKONDARI WAKOSHWA NA HUDUMA ZA AFYA NANE NANE

Posted on: August 6th, 2025

Na WAF, Dodoma


Maonesho ya Nane Nane yameendelea kwa shamrashamra katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, huku wanafunzi wa Shule ya Sekondari Zuzu wakipata fursa ya kutembelea banda la Wizara ya Afya na kujifunza kwa vitendo kuhusu afya bora. 


Furaha na shauku zimeonekana wazi kwa vijana hao walipopewa elimu juu ya namna bora ya kujikinga na malaria, lishe sahihi kwa ukuaji wa mwili na akili, pamoja na matumizi sahihi ya dawa za kufubaza maambukizi ya virusi vya UKIMWI (ARVs).


Mbali na hayo, wamesema elimu waliyopewa kuhusu umuhimu wa chanjo dhidi ya homa ya ini, wakielezwa namna ugonjwa huo unavyoambukizwa na jinsi ya kujikinga.


 Mafunzo hayo yameambatana na mijadala ya wazi, maswali na majibu, huku wataalam kutoka Wizara ya Afya wakitoa ufafanuzi wa kina kwa kila swali lililoulizwa.


Baadhi ya wanafunzi akiwepo Jackline Donard na Daniel Titto wameonesha kufurahishwa kwao na huduma hizo huku wakiahidi kuwa mabalozi wa afya shuleni kwao.


Kwa upande wa mwalimu Bi. Asia Rubaba waliyembatana na wanafunzi hao ametoa pongezi kwa niaba ya wenzake kwa Wizara ya Afya kwa kuandaa banda lenye maudhui ya kujenga taifa lenye afya bora na uelewa mpana kuhusu masuala ya afya ya jamii