Wizara Ya Afya

DKT. SAMIZI AHIMIZA LISHE BORA ILI KUKABILIANA NA UTAPIAMLO

Posted on: March 5th, 2026

Na Shaban K. Juma, WAF-Mbeya

Naibu Waziri wa Afya, Florence Samizi, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapatiwa lishe bora ili kupunguza tatizo la utapiamlo linaloathiri ukuaji na maendeleo ya mtoto.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya, Dkt. Samizi amesisitiza umuhimu wa kuzingatia lishe bora kwa watoto kwa siku za mwanzo wa maisha na akieleza kuwa, kipindi hicho ni msingi wa afya na ustawi wa mtoto.

Amehimiza unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee baada ya mtoto kuzaliwa, akibainisha kuwa maziwa ya mama yana virutubisho muhimu na kinga dhidi ya magonjwa ya utotoni.

Aidha, amesisitiza kuimarishwa kwa huduma za uangalizi kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) ili kupunguza vifo na madhara ya kiafya yanayoweza kujitokeza.

Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi ametoa wito kwa wakuu wa hospitali na wakurugenzi wa halmashauri kuwekeza katika mafunzo ya huduma za dharura kwa watumishi wa afya kupitia vitengo maalum vya mafunzo. Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ujuzi wa watumishi, kuboresha utoaji wa huduma katika vituo vya afya na kupunguza rufaa zisizo za lazima.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa mama na mtoto, kwa lengo la kufikia vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.