WAMILIKI WA MAABARA BINAFSI NCHINI WATAKIWA KUFUATA MIONGOZO, KUWEKA KIPAUMBELE KWENYE UBORA WA HUDUMA
Posted on: August 22nd, 2025
Na. WAF, Mwanza
Msajili wa Maabara Binafsi nchini Bw. Dominic Fwilling’afu amewataka Wamiliki wa Maabara Binafsi kuzingatia ubora wa huduma pamoja na miongozo iliyopo na kuendeleza mazingira rafiki wanapotoa huduma za uchunguzi wa magonjwa kwa wananchi.
Akizungumza leo Agosti 21, 2025 Jijini Mwanza, wakati kikao na wamiliki wa maabara binafsi, Msajili amesema kipaumbele kikuu cha Wizara ya Afya ni kuhakikisha huduma za maabara zinazotolewa nchini zinakuwa bora, salama na zenye kuaminika.
Bw. Fwilling'afu amesema ubora wa huduma hizo ndio msingi wa kujenga jamii yenye afya imara, hivyo ni wajibu wa kila mtaalam wa maabara kuhakikisha matokeo yanayotolewa yanaendana na viwango vya kitaifa na kimataifa.
“Mnatakiwa kujenga ushirikiano na kwenda kujifunza kwenye maabara zinayofanya vizuri zaidi ili kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema Bw. Fwilling'wafu.
Kwa upande wake, Mlezi wa Kanda ya Ziwa kutoka Bodi ya Maabara Binafsi za Afya, Bw. Emanuel Mjema, amesema huduma bora za maabara hazijengwi tu kupitia matokeo ya vipimo, bali zinahitaji kuzingatia miongozo ya kitaifa na masharti ya kisheria, huku wamiliki wakishirikiana na waratibu kuhakikisha wanapata wataalam wenye sifa, maadili na weledi.
“Hatua hizi za pamoja zitasaidia kuongeza imani ya wananchi katika huduma zinazotolewa na maabara binafsi, sambamba na kuhakikisha huduma za afya nchini zinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa," amesema Bw. Mjema,
Msajili kupitia kikao hicho ametoa maelekezo kwa wamiliki wa maabara binafsi za afya kote nchini kutoa huduma bora za maabara kwa kuzingatia miongozo iliyowekwa.