WAHUDUMU WA AFYA WAHIMIZWA KUBORESHA MAWASILIANO KATI YAO NA WATEJA
Posted on: February 29th, 2024
NA: WAF, Morogoro
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Bi. Ziada Sellah, ametoa wito kwa watumishi wa afya kuimarisha mawasiliano baina yao na wateja ili wananchi wanapata huduma zenye heshima na staha, wakizingatia utu wao.
Hayo yameelezwa leo, Februari 29, 2024, Mkoani Morogoro katika kikao kilichowakutanisha wadau mbalimbali kama vile Pathfinder, Americares, na Ifakara Institute, kilichokuwa na lengo la kujadili njia za kuboresha huduma za mawasiliano baina ya watoa huduma na wateja.
Bi. Ziada amewataka wahudumu wa afya kutumia lugha safi na kuhakikisha wateja wanapata huduma zenye heshima na staha, wakizingatia utu wao akisisitiza umuhimu wa mawasiliano mazuri baina ya wahudumu wa afya na wateja wao.
Pia amewahimiza wahudumu wa afya kuzingatia kutoa elimu kwa wateja kuhusu haki na wajibu wao kwani kwa kufanya hivyo itasaidia wateja kupata taarifa zote muhimu wanapofika katika vituo vya afya.
"Napenda kutoa pongezi kwa vyama vya kitaaluma kwa juhudi zao za kutoa elimu kwa wahudumu wa afya, ambayo imechangia katika kufikia lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi," amesema Bi. Ziada.
Kupitia jitihada hizi za kuboresha mawasiliano, Serikali inalenga kuhakikisha kuwa huduma za afya zinakuwa karibu zaidi na zinazoeleweka kwa wananchi, na hivyo kuongeza ufanisi na ubora katika utoaji wa huduma za afya.