Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAGONJWA ZAIDI YA 6000 KUTOKA NJE YA NCHI WAMEPATIWA MATIBABU TANZANIA.

Posted on: March 13th, 2024



Na. WAF, Dar Es Salaam.

Wagonjwa zaidi ya 6000 kutoka nje ya nchi wamepatiwa matibabu katika hospitali ya taifa, taasisi za afya, Hospital za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel leo Machi 13, 2024 katika kipindi maalum cha kurasa 365 za Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema idadi hiyo imeongezeka kutokana na uwekezaji mkubwa wa Miundombinu, vifaa tiba vya kisasa, watumishi, uboreshaji wa Tiba Mtandao, upatikanaji wa dawa na kusomesha wataalam kupita Samia Scholarship uliofanywa ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Uwekezaji wa uliofanyika katika sekta ya afya imeleta Tiba utalii ambapo pia inachangia ongezeko la pato la taifa kwa sababu wagonjwa wanaokuja kutoka Comoro, DRC Kongo na Zaire, Zambia, Malawi, Kenya na Uganda kwa ajili ya kufuata huduma za matibabu ambapo hapo awali walikuwa wakienda nchi za ulaya na India” amesema Dkt. Mollel

Aidha ameongeza kuwa Watoto saba wenye ugonjwa wa Selimundu washapatiwa matibabu ya kupandikiziwa Uroto katika Hospitali ya Kanda ya kati ya Benjamini Mkapa.

“ Sasa hivi tumeweza kuokoa maisha ya Watoto waopoteza maisha kwa ugonjwa wa Selimundu kwa kuwa na huduma ya upandikizaji wa Uroto katika Hospitali ya Benjamini Mkapa.” Ameeleza.

Mwisho. Dkt. Mollel amewata watumishi katika sekta ya afya nchi kufanya kazi kwa weledi na kujitika kutoa huduma bora kwa watanzania.

“Wataalamu wa Afya hatumdai Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu yeye kashafanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya Afya kilichobaki ni sisi kumlipa kwa kufanya kazi kwa bidii sisi tunadeni la kulipa uwekezaji huo kwa kutoa huduma bora kwa Watanzani” Amesema Dkt. Godwin Mollel Naibu Waziri wa Afya.