Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAGONJWA HAWAENDI HOSPITALI KUSHANGAA MAJENGO, BALI HUDUMA BORA- PROF. MASELE

Posted on: December 8th, 2021

Mwenyekiti wa Bodi ya usajili ya Wauguzi na Wakunga nchini, Prof. Lilian Masele, amewaambia wauguzi zaidi ya 1200, ambao wametunukiwa vyeti vyao kuwa, wagonjwa hawaendi hospitani kwa ajili kushangaa majengo, bali wamefuata huduma bora za afya.

Akihutubia kwenye Mahafali ya tatu ya baraza la Wakunga na Wauguzi yaliyofanyika hii leo jijini Dodoma, Masele amesema, ipo dhana iliyojengeka miongoni mwa watoa huduma kudhani kuwa, wagonjwa hufika hospitalini na kwenye vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya kushangaa majengo kitu ambacho kinadumaza huduma kwa mteja na kufanya vituo vingi kukimbiwa na wagonjwa.

“Msingi Mkuu wa kazi zetu ni weledi (Professionalism), hivyo kila mmoja wetu atambue anao wajibu wa kuhakikisha anakwenda kuitendea haki taaluma hii kwa kutekeleza wajibu wake kwa juhudi, weledi na maarifa bila kusahau miiko inayo ongoza taaluma hii muhumu kwa mustakabali wa taifa” Amesema Prof. Masele.

Prof. Masele amewataka wahitimu hao, kuzingatia masomo waliyokumbushwa siku ya mahafali juu utendaji wa kazi, ikiwepo miongozo, sheria ya uuguzi, umuhimu wa kujiendeleza kielimu na kujua muundo wa baraza la Wauguzi na Wakunga na jinsi baraza hilo litakavyo weza kuwasaidia wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Awali, akitoa salaam za Baraza la Wauguzi na wakunga nchini kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Msajili wa baraza Bibi, Agnes Mtawa, alisema shabaha ya Mahafali hayo ambayo yanafanyika kwa mara ya tatu, ni kukutana na kukumbushana majukumu kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

“Hii ni mara ya tatu tunafanya mahafali, lakini kwa siku ya leo tumefanya tofauti kidogo, Wauguzi na Wakunga hawa, baada ya kufanya mitihani ya Bodi ya Baraza la Wauguzi   na kufaulu, tumeona ni vema tuwaite pamoja na kuwakumbusha wajibu wao, hivyo kuanzia mapema tulikuwa tunafundishana nini tunatakiwa kwenda kutekeleza katika majukumu yetu.” Alisema Mtawa.

Jumla ya wauguzi na wakunga kutoka makundi ya waliopo makazini na wale wasiokuwepo na kazi, wapatao 1224, wametunukiwa Vyeti na Leseni za Uuguzi na Ukunga wakiwepo waliosajiliwa kwa Shahada (29), Astashada (1096), Stashada (99).