Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAGANGA WA TIBA ASILI/MBADALA WAHIMIZWA KUJISAJILI KATIKA BARAZA LA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA.

Posted on: August 26th, 2022


Na. Waf. Morogoro

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Urio Kusirye amewahimiza waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini kuzisajili dawa na vituo vyao katika Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ili ziweze kurasimishwa.

Hayo ameyasema leo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yanayifanyika Mkoani Morogoro

Dkt. Kusirye amesema wanaposajili dawa na vituo vyao itawasaidia kufanya kazi kwa uhuru ikiwa ni kutoa huduma za Tiba Asili katika mahospitali.

"Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala wapo hapa, sajilini vituo na dawa zenu ili ziweze kurasimishwa na kuwa rasmi" amesema Dkt. Kusirye.

Kwa upande mwingine Dkt. Kusirye amewasihi waganga hao kutojihusisha na imani potofu pamoja na kutoa matangazo yasiyofaa kwenye mitandao ya kijamii.

"Msitie matangazo yasiyofaa ambayo hayana vibali kutoka baraza la tiba asili na tiba mbadala mnapaswa kufuata sheria za baraza hili" amesema Dkt. Kusirye.

Hata hivyo Dkt. Kusirye amezitaka halmashauri kutenga maeneo yenye mitidawa iliyopandwa, na kuwahamasisha waganga wa tiba asili kupanda na kuhifadhi mitidawa katika maeneo yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili/Tiba Mbadala Wizara ya Afya Dkt. Paul Mhame amesema katika maadhimisho haya Watanzania watapata elimu mbalimbali kuhusu Tiba asili na Tiba Mbadala na kuwaalika wananchi wa Mkoa wa Morogoro na wa Mikoa jirani kushiriki katika maadhimisho hayo ili kutangaza mila na desturi za tiba na kupata elimu kuhusu Tiba Asili.

MWISHO.