Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAFAMASIA WAELEKEZWA KUBORESHA NAMNA YA UAGIZAJI DAWA KULINGANA NA UHITAJI KWA JAMII.

Posted on: September 13th, 2023

NA WAF- DSM


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewaelekeza Wafamasia katika ngazi zote kuhakikisha wanaagiza dawa kulingana na aina ya magonjwa yanayoisumbua jamii yao pamoja na mzigo wa wagonjwa, ili kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa dawa kwa wananchi katika vituo vya kutolea huduma. 


Dkt. Mollel amesema hayo katika ziara ya kamati ya Bunge ya kudumu ya Afya na masuala ya UKIMWI ilipotembelea katika ofisi za Bohari ya Dawa Jijini Dar es Salaam ili kujionea shughuli mbalimbali za utendaji katika taasisi hiyo yenye majukumu ya ununuzi wa dawa, usambazaji pamoja na utengenezaji. 


Ameendelea kwa kutoa wito kwa Wabunge kwa kushirikiana na madiwani katika majimbo yao kufuatilia kwa ukaribu masuala ya dawa katika vituo vyao vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha suala la dawa litakuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya Halmashauri kwani ndio yanayomgusa Mtanzania kwa karibu zaidi pindi anapoumwa.


Nae, Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Bw. Mavere Tukai amesema, Bohari ya Dawa ipo kwenye utekelezaji wa mikakati iliyojiwekea ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa vituo vyote pamoja na ujenzi wa maghala mapya ikiwemo maghala mawili yanayojengwa Jijini Dodoma na Mtwara. 


Ameendelea kusema kuwa, tayari MSD imewasilisha maombi ya fedha ili kukuza mtaji utaowasaidia kutoa huduma bora kwa vituo vya kutolea huduma ili wananchi wanufaike na huduma hizo.