Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

VIONGOZI MUWAJIBIKE KUTATUA KERO ZA WANANCHI, MSISUBIRI MPAKA AJE WAZIRI MKUU

Posted on: February 28th, 2024



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Viongozi na Watendaji ngazi ya Mikoa na Wilaya kuwajibika ipasavyo kusimamia Sekta ya Afya na kutatua kero za wananchi zinazorudisha nyuma upatikanaji wa huduma za afya na wasisubiri mpaka Viongozi wa juu kufika na kubaini changamoto.

Waziri Mkuu ameyasema hayo akiwa katika ziara Mkoa wa Mara wakati akisalimiana na wananchi wa Halmshauri ya Wilaya ya Tarime ambapo amesema ishara ya kelele za wananchi juu ya changamoto katika upatikanaji wa huduma za afya ni kiashiria cha kuwa kuna changamoto.

“Hatutarajii mwananchi aende Hospitali, halafu aandikiwe cheti aambiwe nenda kanunue dawa kulee, Kama kelele za wananchi ziko hivi liko tatizo". Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Mhe. Majaliwa amesisitiza uwajibikaji wa viongozi kwa kutembelea katika Vituo vya kutolea huduma za afya ili kukagua hali ya utoaji wa huduma za afya ili kubaini changamoto na kuzifanyia kazi.

Hata hivyo, Waziri mkuu amesema Serikali itaendelea kutoa fedha katika kila Halmashauri nchini ili kuweza kuboresha huduma za afya hivyo ni wajibu wa watendaji kusimamia fedha hizo ili zitumike kama zinavyohitajika.