Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA SONGWE UKAMILIKE NDANI YA MIEZI SITA

Posted on: September 13th, 2023

Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe ukamilike ndani ya miezi Sita hasa jengo la mama na mtoto, jengo la wagonjwa wa dharura (EMD) na jengo la wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU) ili wananchi wapate huduma haraka na kwa urahisi.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo Septemba 13, 2023 alipokuwa anaongea na watumishi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe akiwa kwenye ziara yake ya kukagua utolewaji wa huduma, upatikanaji wa dawa pamoja na mradi wa ujenzi katika Hospitali hiyo.


“Fedha zimetolewa kwa nini ujenzi unachelewa, Sasa nataka ujenzi huu ukamilike hasa jengo la mama na mtoto, EMD na ICU ndani ya miezi Sita”. Amesema Waziri Ummy 


Waziri Ummy amepongeza kukamilika kwa jengo la Maabara ambalo limekamilika kwa asilimia 100 na kuanza kufanya kazi katika Hospitali hiyo. 


Aidha, Waziri Ummy amesema Hospitali zote za Rufaa za Mikoa ziwe na madaktari bingwa ili kusaidia huduma za kibingwa zinapohitaji katika Hospitali husika.


“Tutawapeleka madaktari bingwa katika kila Hospitali za Rufaa ya Mikoa ili waweze kusaidia huduma za kibingwa lakini pia madaktari wote watalipwa sawa na daktari aliyopo Muhimbili kwa kuwa wote ni sawa na wamesoma kitu kimoja”. Amesema Waziri Ummy