Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

UGONJWA USIOJULIKANA KAGERA WABAINIKA KUWA NI UGONJWA WA MARBURG

Posted on: March 22nd, 2023

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema uchunguzi wa Maabara ya Taifa umethibitisha uwepo wa virusi vya Marburg ambavyo vinasababisha ugonjwa wa Marburg Virus Disease (MVD) katika Mkoa wa Kagera ambao umesababisha vifo vya Watu watano hadi sasa ambapo amesema Ugonjwa huo hauna tiba mahususi bali hutibiwa kwa dalili anazokuwa nazo Mgonjwa.


Akiongea leo Dar es salaam, Ummy amesema “Uchunguzi ambao tumeufanya katika Maabara yetu ya Taifa ya Afya ya Jamii umethibitisha uwepo wa virusi vya Marburg ambavyo vinasababisha ugonjwa unaojulikana kama Marburg Virus Disease(MVD)”


“Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huu wa Marburg uligundulika kwa mara ya kwanza Ujerumani mwaka 1967 katika Mji wa Marburg na ndio asili ya jina la ugonjwa huu, ugonjwa huu ulishawahi kuripotiwa katika Nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya”


“Ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa Binadamu mmoja kwa mwingine hususani kwa njia ya kugusa majimaji ambayo yanaweza kuwa mate , mkojo, damu, machozi au kinyesi yatokayo kwenye maiti au Mgonjwa mwenye dalili, maambukizi pia yanaweza kutoka kwa Wanyama kwenda kwa Binadamu iwapo Mtu atakula au kugusa mizoga au Wanyama walioambukizwa”


Itakumbukwa siku tano zilizopita Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitoa tahadhari juu ya uwepo wa ugonjwa ambao bado ulikuwa haujajulikana Mkoani Kagera katika Wilaya ya Bukoba Vijijini ambapo Watu 7 walisadikika kupata dalili za homa, kutapika, kutokwa damu maeneo mbalimbali ya mwili na figo kushindwa kufanya kazi na Watu watano kati yao wakaripotiwa kufariki.