Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

TUMIENI TAFITI ZA KISAYANSI KWA AJILI YA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: September 22nd, 2023

Na WAF - MBEYA


Taasisi za kitafiti nchini zimetakiwa kutumia tafiti za kisayansi katika kupata taarifa sahihi na kufanya maamuzi ili kuimarisha na kuboresha huduma za afya nchini.


Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Dkt. Hamad Nyembea aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali kwenye kongamano la tano la afya na utafiti wa masomo lililozikutanisha Taasisi za NIMR, HJFMRI, UDSM, PEPFAR, WRAIR, BAYLOR , MHRP mkoani Mbeya.


Dkt. Nyembea amesema tafiti za kisayansi zinasaidia katika kutoa taarifa sahihi na kupelekea kutoa maamuzi ambayo yataisaidia serikali katika kuboresha huduma za afya nchi.


“Serikali imewekeza kwa Kiasi kikubwa kwenye Sekta ya Afya, Kuongeza vituo vya watoa Huduma 

ambavyo vimeongezeka kwenye miaka mitatu iliyopita. Kipaumbele kikubwa cha serikali ni kutoa Huduma Bora. Ubora wa Huduma utapatikana ikiwa tutapata Taarifa sahihi ambazo zitasaidia serikali kufanya maamuzi sahihi ili kuweza kuboresha huduma hizo”. Amesema Dkt. Nyembea.


Aidha, Dkt. Nyembea amesisitiza kuendelea kufanyika kwa tafiti mbalimbali za kisayansi nchini kwa kuwa lengo la kuimarisha na kuchangia kuboresha huduma za afya kwa wananchi.


“Lengo la Kongamano Hili ni kuchangia vitu ambavyo vimeweza kupatikana kwenye tafiti mbalimbali za kisayansi. Kwa kupitia sayansi tunahitaji Kufanya tafiti nyingi ambazo zitatupa matokeo mazuri na taarifa sahihi kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi". Amesema Dkt. Nyembea.


Hata hivyo amesema kuwa huduma zinazotakiwa kutolewa katika kituo cha kutolea huduma za afya ziwe ni za uhakika, nzuri na bora kwa wananchi hivyo kutomlazimisha kutoka kituo kimoha kwenda kingine kwa ajili ya kukamilisha huduma anazotaka.


“Tunapoonyesha Upande wa Huduma tunamaanisha kwamba kituo kikifunguliwa kiwe na Kila Huduma iwezekenavyo ili mteja akienda akamilishe matibabu kuliko kuhama kituo kimoja kwenda kingine kwa ajili ya kukamilisha matibabu”. Amesisitiza Dkt. Nyembea.