SIMAMIENI MPANGO WA MMS KWA KUZINGATIA MAHITAJI YA WAJAWAZITO
Posted on: August 22nd, 2025
Na WAF - Dodoma
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amemtaka Mkurugenzi wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Dkt. Ahmad Makuwani pamoja na viongozi wengine wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI, kusimamia Mpango wa kuanzishwa matumizi ya virutubishi lishe kwa uadilifu, umahiri na kwa kuzingatia mahitaji ya wajawazito hapa nchini.
Dkt. Grace ametoa maelekezo hayo Agosti 20, 2025 kwenye kikao chenye lengo kuu la kuongeza kasi ya uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi na lishe kwa akina mama wajawazito nchini ambao utajumuisha kuanzishwa kwa matumizi ya virutubishi vya nyongeza kilichofanyika mkoani Dodoma.
Aidha, Dkt. Magembe amesema Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi za kwanza Duniani kutambua njia bora ya kuimarisha huduma za lishe pamoja na kutoa virutubishi vya 'Multiple Micronutrient Supplements' (MMS), hivyo kuifanya nchi kuwa mfano wa rejea kwa nchi nyingine katika eneo hilo.
"Katika utekelezaji wa lengo hilo, naelekeza pia kikao hiki kitumike katika kujengeana uelewa wa pamoja kuhusiana na umuhimu wa kuboresha huduma za lishe kwa wajawazito ikiwemo uandaaji wa chakula na mpangilio sahihi wa mlo na sio tu utoaji wa virutubishi vya lishe," amesema Dkt. Magembe.
Pia, ameelekeza kikao hicho kijadili kwa kina na kukubaliana juu ya mbinu na namna bora ya kuandaa na kutekeleza mpango huo wa Kitaifa ili uwe endelevu ikiwemo ushiriki wa sekta binafsi katika kuzalisha virutubishi hivyo, kupitia viwanda vya ndani na kuhakikisha taarifa za utekelezaji zinawasilishwa kila baada ya miezi miwili ili kufahamu hatua zilizofikiwa.