SERIKALI YAPIGA HATUA UENDELEZAJI HUDUMA ZA AFYA UTENGAMAO NCHINI
Posted on: September 16th, 2025
NA WAF - DAR ES SALAAM
Serikali ya Tanzania imepiga hatua katika uendelezaji wa huduma ya afya ya utengamao tofauti na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma ikiendeleza jitihada zake za kuimarisha huduma hiyo kwa kuhakikisha wananchi wanapata uelewa kuhusu huduma hiyo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Rehab Health Tanzania, taasisi ya kuelimisha kuhusu huduma za utengamao na haki za watu wenye ulemavu, Profesa Lawrence Museru Septemba 12, 2025, wakati akifunga Kongamano la Tatu la Utengamao lililofanyika kwa siku tatu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa jijini Dar es Salaam.
"Hali ilivyokuwa wakati tunaanza kushughulikia masuala ya utengamao, kuna maendeleo makubwa. Tulipokuwa tukiwaambia watu waende Hospitali ya Muhimbili kwa Mama Cheza, alikuwa ni mtu pekee akitoa huduma ya tiba ya utengamao, watu wengi hawakujua hata walikuwa wanaenda kufanya nini," amesema Prof. Museru.
Ameongeza kuwa ili kuendeleza tiba ya utengamao, wataalam wanapaswa kukutana na kuendelea kujifunza mara kwa mara, kwani bado idadi ya wataalam wa utengamao ni ndogo ukilinganisha na uhitaji uliopo.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba Wizara ya Afya Dkt. Mwinyi Kondo amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inafanya juhudi kuhakikisha huduma ya utengamao inapatikana kwa urahisi na inakidhi mahitaji ya kila mtu.
"Serikali inatoa ufadhili kwa madaktari kwenda kusoma na kujiendeleza, na kozi ya utengamao imepewa kipaumbele kikubwa kuanzia ngazi ya msingi. Kwa mtu anayekwenda kusomea Stashahada ya Utengamao, anapata mkopo kutoka Serikalini," amesema Dkt. Kondo.
Kongamano hilo la tatu la Utengamao limewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya kwa lengo la kupata elimu kuhusu namna ya kutoa huduma za utengamao kwa wananchi, huku likitoka na maazimio sita ya namna ya kukabiliana na uhaba wa wataalam uliopo.