Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAJIZATITI KUTATUA TATIZO LA AFYA YA AKILI MAHALA PA KAZI.

Posted on: October 9th, 2024

Na WAF – Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kuhakikisha kuwa mahali pa kazi panakuwa salama na kuongeza tija kwenye maeneo ya kazi kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta

Hayo yamesemwa Oktoba 10, 2024 na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Dkt. Ahmad Makuwani akiwa amemuwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ufunguzi wa semina kwa viongozi na maafisa utumishi kwenye Maadhimisho ya siku ya afya ya akili duniani iliyofanyika kitaifa jijini Dodoma ikiwa imebebwa na kauli mbiu “Ni wakati wa kulipa kipaumbele afya ya akili mahala pa kazi”

“Dhamira kuu ya maadhimisho ya mwaka huu ni kuhakikisha kwamba afya ya akili inakuwa sehemu muhimu ya ajenda za mwaka mahali pa kazi. Tunataka waajiri na waajiriwa waweke mipango inayopunguza visababishi vya magonjwa ya akili na kuhakikisha utambuzi wa mapema na matibabu na kufanya mahala pa kazi kuwa salama, na pasipo na vichocheo vinavyoweza kuathiri afya ya akili ya wafanyakazi,” ameongeza

Dkt. Makuwani ametoa wito kwa jamii na wadau kushirikiana na Serikali ili kuweza kutimiza lengo la kuimarisha afya ya akili mahala pa kazi na jamii kwa ujumla kwa ustawi endelevu wa nchi na mtu mmoja mmoja.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Tiba Dkt. Hamad Nyembea amesema upatikanaji wa huduma za afya ya akili umeanza na mikakati madhubuti ya serikali kufikisha huduma hizo katika ngazi ya Halmashauri na kuhakikisha hadi kufika 2030 kuona huduma hizo zimefika ngazi ya chini.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe Dkt. Paul Lawala ameeleza kufuatia kauli mbiu ya maadhimisho ya afya ya akili ni kulenga mahala pa kazi ni jukumu la viongozi wanaosimamia rasilimali watu kulinda afya ya akili binafsi na watumishi na kujua changamoto za tatizo hilo na kuzishughulikia kwa njia Chanya kwa kuepuka kuwatenga, kuwaadhibu, kuwanyanyapaa watumishi wenye changamoto ya afya ya akili.