SERIKALI YAENDELEA KUTAFUTA WADAU KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Posted on: February 5th, 2026Na WAF - Geneva, Uswisi
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, ameendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kufanya kikao na wadau wa afya kutoka shirika la Global NCD Alliance, kilichofanyika pembezoni mwa mikutano ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Dkt. Magembe ametoa shukrani kwa shirika hilo kwa ushirikiano uliopo, hususan mchango wake katika utoaji wa vifaa tiba vya magonjwa yasiyoambukiza vilivyotumika katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini, hasa katika ngazi ya msingi.
Aidha, Dkt. Magembe ameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha huduma za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza zinaimarishwa na kuwa endelevu, ikiwemo mkakati wa kujenga uwezo wa vituo vya afya ya msingi ili kutoa huduma bora na za mapema kwa wananchi.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano na wadau wa kimataifa katika kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza nchini, akieleza kuwa juhudi hizo ni muhimu katika kulinda afya ya wananchi na kupunguza gharama za matibabu kwa familia na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wao, wadau wa Global NCD Alliance wakiongozwa na Mkuu wa Shirika la hilo Bi. Joanna Laurson, waliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutafuta rasilimali fedha, vifaa na Kutoa mafunzo kwa watumishi na misaada zaidi itakayosaidia kuimarisha huduma za kinga, uchunguzi wa mapema na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza nchini.