DKT. MAGEMBE AKUTANA NA UJUMBE WA SERIKALI YA WATU WA CHINA
Posted on: February 6th, 2026Na WAF - Geneva, Uswisi
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, umeendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya kwa kufanya vikao na wadau mbalimbali pembezoni mwa Mkutano wa 158 wa Bodi Tendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoendelea jijini Geneva, Uswisi.
Leo Februari 05, 2026, Dkt. Magembe alikutana na ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ulioongozwa na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa, Dr. Ding Yang ambapo katika kikao hicho, Dkt. Magembe aliishukuru Serikali ya China kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha huduma za afya nchini.
Dkt. Magembe alieleza umuhimu wa upanuzi wa Hospitali ya moyo ya JKCI, kuwezesha matumizi ya reli ya TAZARA katika utoaji wa huduma za Afya na kukuza tiba utalii kwa jamii zinazopitiwa na reli hiyo pamoja na wananchi kutoka nchi jirani.
Aidha, Dr Magembe aliongelea mpango wa kujenga kituo cha umahiri cha kukabiliana na magonjwa ya dharura ya mlipuko katika Kanda ya Ziwa mkoani Kagera.
Kwa upande wake, Dr. Ding Yang ameelezea dhamira ya Serikali ya China kuendelea kushirikiana na Tanzania na kuahidi kutuma timu ya wataalam nchini Tanzania siku chache zijazo kwa ajili ya kufanya tathmini ya kitaalamu kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo na kuandaa mpango wa pamoja wa utekelezaji.
Aidha, Dr. Yang amesema kuwa Serikali ya China ina mpango wa kuandaa mkutano wa pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa WHO utakaofanyika mwezi Mei 2026 unaolenga kujadili matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence) katika sekta ya afya, na kwamba China itawasilisha ombi kwa Serikali ya Tanzania kuwa mdhamini mwenza (Co-sponsor) wa mkutano huo.